Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akiangalia emwani (kahawa ya asili) aliyooneshwa na Makamu Mwenyekiti wa Buhaya Festival, Nancy Kazaura, kwenye tamasha hilo lililofanyika katika ukumbi Mlimani City jijini Dar es Salaam, Oktoba 27, 2024. Kutoka kushoto ni Mlezi wa Tamasha hilo na Mkuu wa Mkoa wa Kagera Hajat. Fatma Mwasa. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu).
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akizungumza kwenye tamasha la Buhaya Festival lililofanyika katika ukumbi Mlimani City jijini Dar es Salaam, Oktoba 27, 2024. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
Washiriki wa Tamasha la Buhaya Festival ambao ni wana Kagera, wakimsikiliza Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akizungumza kwenye tamasha hilo lililofanyika katika ukumbi Mlimani City jijini Dar es Salaam, Oktoba 27, 2024. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu).
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akimkabidhi Mke wa Sir. George Kahama, Janeth Kahama cheti cha utambuzi wa kua kinara wa ubunifu na uongozi kijamii na malezi ya vijana, kwenye tamasha la Buhaya Festival lililofanyika katika ukumbi Mlimani City jijini Dar es Salaam, Oktoba 27, 2024. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu).
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akiwa amevaa kofia na kushika bakora zinatumika na jamiii ya asili ya watu wa Kagera kwenye tamasha la Buhaya Festival lililofanyika katika ukumbi Mlimani City jijini Dar es Salaam, Oktoba 27, 2024. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu).
………….
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amewataka Watanzania wahakikishe wanalinda utamaduni na kujenga misingi ya kuhamasisha vijana na vizazi vijavyo kutambua na kuenzi historia na urithi wa Mtanzania.
Amesema kuwa ni wajibu wa kila Mtanzania kutunza utamaduni, mila na desturi kwa sababu utamaduni ni nguzo ya utambulisho wa jamii husika na ni muhimu kwa kizazi kijacho.
Amesema hayo leo (Jumapili, Oktoba 27, 2024) wakati akifungua Tamasha la Buhaya 2024 ‘Buhaya Festival’ lililofanyika katika ukumbi wa Mlimani City, jijini Dar es Salaam.
“Katika siku za sasa, ambapo teknolojia na utandawazi vinazidi kuimarika, ni rahisi kupoteza mila na desturi zetu, hivyo tunaposhiriki tamasha hili, tunajifunza na kuhamasisha jamii zetu kuhusu umuhimu wa urithi wetu wa kiutamaduni.”
Kadhalika, Mheshimiwa Majaliwa amewaasa wazazi, jamii na madhehebu ya dini kuendelea kuhimiza utunzaji wa maadili kwa kuzingatia mila na desturi ili kuepuka mmomonyoko wa maadili kwa vijana na jamii kwa ujumla.
“Watanzania wote tuendelee kuheshimu na kuenzi tamaduni zilizo nzuri kama njia ya kuimarisha umoja, mshikamano na maendeleo ya kiuchumi,” amesisitiza.
Katika hatua nyingine, Mheshimiwa Majaliwa ameagiza Mikoa yote nchini kwa kushirikiana na mashirika yasiyo ya kiserikali na sekta binafsi iweke mipango ya kuandaa matamasha ya utamaduni kuanzia ngazi za Wilaya ili kuendeleza na kuhifadhi vivutio, mila na desturi za maeneo husika.
Akizungumzia kuhusu Maendeleo ya Mkoa wa Kagera, Mheshimiwa Majaliwa amesema kuwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ameendelea kutoa fedha kwa ajili ya utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo katika mkoa huo kwenye sekta za nishati, maji, kilimo, uvuvi, Uchukuzi na ujenzi wa barabara.
Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Kagera, Fatma Mwassa amesema kuwa tamasha hilo linalowaleta pamoja Wana-kagera,linalenga kulinda na kutangaza Utamaduni, mila na desturi za Wana-Kagera pamoja na kutangaza vivutio na fursa zilizopo mkoa wa Kagera.
“Buhaya inaendelea kukumbukwa kwa maadili ushirikiano na ujasiri uliojengwa na wazee wetu, pia kupitia tamasha hili mkoa umetangazwa sana, mila na deturi zimeenziwa”
Naye, Mwenyekiti wa Tamasha hilo, Wilson Kazaura amesema kuwa tamasha hilo ni zaidi ya burudani kwani linatoa fursa kwa jamii ya Wahaya kuungana, kujifunza na kuhifadhi urithi wa kitamaduni kwa vizazi vijavyo
“Tutaendelea kushikamana na Serikali katika kuenzi tamaduni ili tuweze kuzirithisha kwa vizazi vijavyo na tutaendelea kuenzi sanaa, mila na desturi ambao ni utambulisho wetu”.