Na Prisca Pances
ILI kuimarisha uhusiano wa kihistoria kati ya Tanzania na India,Kamishna Mkuu wa India nchini Tanzania Bishwadip Dey ameanzisha mpango ‘Karibu Vijana wa Tanzania,’ uliolenga kuwashirikisha wanafunzi wa Kitanzania, kutwaa maarifa kuhusu utamaduni wa India na jukumu ya kiongozi huyo katika kukuza ushirikiano wa kimataifa.
Awali katika uzinduzi wa mpango huo amewakaribisha wanafunzi 30 kutoka Shule ya Sekondari ya Kimataifa ya Kitaaluma, Dar es Salaam, kwenye ofisi za Ubalozi huo.
Uzinduzi huo umefanyika juzi katika ofisi za Ubalozi wa India nchini Tanzania dar es salaam
Asema mpango huo umelenga kuboresha jukwaa la mwingiliano kwani wanafunzi wamepata nafasi ya kuchunguza majukumu ya kidiplomasia na kujifunza kuhusu mchango wa Kamishna Mkuu katika kuimarisha uhusiano wa India na Tanzania.
“Malengo yetu ni kuwahamasisha wanafunzi wa Kitanzania kuwa marafiki wa India, ambao wanaweza kushiriki kile walichojifunza kuhusu India na uhusiano wake na Tanzania. Tunaamini kuwa kupitia mipango kama hii, tunajenga madaraja ya urafiki na ushirikiano ambayo yatadumu kwa vizazi vingi.”alisema Dey
Akimwakilisha Mkuu wa Shule ya Kitaaluma ya Kimataifa ,Simon Hussein ametoa shukrani kwa ubalozi huo kwani wanafunzi hao wamejifunza vitu vingi.
“Tunashukuru kwa fursa hii ya kielimu kwani wanafunzi wetu wametembelea Kamishna Mkuu, kujifunza kuhusu kazi yake muhimu, na hata kufurahia chakula cha Kihindi. Mpango huu umewapa uelewa wa moja kwa moja kuhusu uhusiano wa kina kati ya nchi zetu mbili.”alisema Hussein
Mmoja wa wanafunzi walioshiriki mpango huo, Nakiete Mlaki, amesema matembezi hayo yalikuwa muhimu sana katika kuongeza uelewa kwani wameona jinsi ilivyo muhimu kwa India na Tanzania kuwa na uhusiano huo hasa katika kukuza biashara, elimu, na kubadilishana tamaduni.
Mafunzo hayo yameyotolewa na maafisa wa Kitanzania kwa kutumia lugha ya Kiswahili, yakilenga mwanga juu ya jukumu la ujumbe huo katika kujenga uhusiano wa kidiplomasia, kiuchumi, na kitamaduni.
Wanafunzi wamejifunza kuhusu ushirikiano wa muda mrefu kati ya India na Tanzania katika sekta za afya, teknolojia, elimu, na biashara—nyanja muhimu za ushirikiano ambazo zimeleta manufaa kwa mataifa yote mawili.
Pia Wanafunzi hao walipata fursa kushuhudia mchakato wa kutoa hati ya kusafiria unavyofanyika hadi kukamilika.
Mpango wa “Karibu Vijana wa Tanzania” sasa utaandaliwa kila mwezi, ukitoa nafasi kwa wanafunzi wa Kitanzania kutembelea ubalozi wa India , kujifunza kuhusu utamaduni wa India, na kupata uelewa kuhusu jukumu la ujumbe wa kidiplomasia katika kukuza urafiki wa kimataifa.