Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali Lela Mohamed Mussa akijibu Maswali yalioulizwa na Waandishi wa Habari kuhusiana na Mafanikio ya Sekta ya Elimu kwa Kipindi cha Miaka Minne (4)ya Uongozi wa Rais Dk Hussein Ali Mwinyi katika Kipindi maalum ZBC TV Mnazi mmoja Zanzibar.
Na Rahma Khamis Maelezo 28/10/2024
Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar Mhe Lela Mhamed Mussa amesema bajeti ya maendeleo ya elimu imeongezeka kutoka bilioni kumi na tisa mwaka 2020 hadi kufikia bilioni mia Tano kumi na nane mwaka 2024.
Ameyasema hayo katika Ukumbi wa ZBC Mnazimoja wakati akielezea mafanikio ya sekta hiyo ikiwa ni shamrashamra za kutimiza miaka minne ya Dkt Hussein Mwinyi
Amesema kuwa ongezeko hilo linatokana na jitihada za Serikali katika kuboresha Sekta ya elimu kwa kujenga Skuli za kisasa katika maeneo yote Unguja na Pemba ili kuleta mageuzi katika sekta hiyo.
Amefahamisha kuwa ufaulu wa wanafunzi umeongezeka kutoka asilimia 25 Hadi kufikia 55 kwa darasa la saba na kutoka asilimia 55 Hadi kufikia asilimia 85.6 kwa wanawanafunzi wa darasa la kumi na mbili kwa mwaka 2023.
Amesema jumla ya madarasa 2,773 yamejengwa na serikali kwa kipindi cha miaka minne huku madarasa mengine mapya 2,037 ikiwemo skuli 26 za gorofa na skuli za chini 53 ujenzi wake umeanza kupitia bajeti ya mwaka wa fedha 2024-2025.
Akizungumzia suala la ajira Waziri Lela amesema kuwa Wizara imefanikiwa kuajiri walimu 73 kwa kwa upande wa mahitaji maalum na kujenga vyuo vya Amali vitano Unguja na Pemba ili vijana waweze kujiajiri.
Hata hivyo amewataka wazazi na walezi kushirikiana na waalimu ili kujenga mustakabali mwema kwa wanafunzi wao