Rais Mstaafu Dkt. Jakaya Kikwete ameshiriki Mkutano wa Bodi wa Taasisi ya Kimataifa inayojishughulisha na Masuala ya Maji Barani Afrika (Global Water Partnership – Southern Africa and Africa Coordination Unit – GWPSA – Africa) uliofanyika tarehe 29 Oktoba, 2024, jijini Pretoria, Afrika Kusini.
Rais Mtaafu Dkt. Kikwete ni Mwenyekiti wa Bodi ya Taasisi hiyo inayotoa msaada wa kitaalamu kwa nchi za Afrika katika kutekeleza programu za usimamizi wa rasilimali za maji, usalama wa maji pamoja na masuala ya mabadiliko ya tabianchi.
Chini ya mwongozo wa Bodi hiyo, Taasisi ya GWPSA – Africa pia inaunga mkono jitihada zinazofanywa na Serikali za nchi za Afrika katika kukusanya fedha za kuimarisha uwekezaji katika sekta ya maji katika nchi husika kupitia Kampeni ya Jopo la Viongozi la Programu ya Uwekezaji katika Sekta ya Maji Barani Afrika (International High-Level Panel on Water Investments for Africa, AIP).
Kampeni hiyo imelenga kukusanya takribani Dola za Marekani bilioni 30 ili kuziba pengo lililopo katika kufadhili miradi ya maji katika nchi mbalimbali za Afrika. Tanzania bara na Zanzibar ni baadhi ya wanufaika wa programu zinazotekelezwa na GWPSA – Africa.
Mbali na kuwa Mwenyekiti wa Bodi ya GWPSA, Rais Mstaafu Kikwete pia ni Mwenyekiti Mwenza Mbadala wa Jopo hilo la Viongozi (AIP) linaloongozwa na Marais wa Senegal, Namibia na Uholanzi.
Akiwa Afrika Kusini, Dkt. Kikwete anatarajia pia kufikisha ujumbe kwa Serikali ya Afrika Kusini kuhusu utayari wa Taasisi ya GWPSA – Africa kusaidia na kufanya kazi kwa pamoja na nchi hiyo inayotarajiwa kushirikiana na Kamisheni ya Umoja wa Afrika kuwa mwenyeji wa Mkutano wa Kampeni ya AIP utakaofanyika mwaka 2025.