Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Rais Mha. Cyprian Luhemeja akifungua kikao cha Makatibu Wakuu cha Maandalizi ya Mkutano wa 29 wa Nchi Wanachama wa Umoja wa Mataifa wa Mabadiliko ya Tabianchi (COP 29), uliofanyika Oktoba 29,2024
mkoani Dodoma.
Naibu Katibu Mkuu (Muungano) Ofisi ya Makamu wa Rais, Bw. Abdallah Hassan Mitawi akizungumza katika kikao cha Makatibu Wakuu cha Maandalizi ya Mkutano wa 29 wa Nchi Wanachama wa Umoja wa Mataifa wa Mabadiliko ya Tabianchi
(COP 29) kilichoanyika Oktoba 29,2024 mkoani Dodoma.
Mkurugenzi wa Mazingira, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Bi. Kemilembe Mutasa akizungumza katika kikao cha Makatibu Wakuu cha Maandalizi ya Mkutano wa 29 wa Nchi Wanachama wa Umoja wa Mataifa wa Mabadiliko ya Tabianchi (COP 29) kilichoanyika Oktoba 29,2024 mkoani Dodom.
………….
Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Rais Mhandisi Cyprian Luhemeja amesema suala la mazingira ni mtambuka hivyo linahitaji ushirikiano kutoka wizara, taasisi pamoja na wadau ili kuhakikisha sekta hiyo inakuwa endelevu.
Amesema hayo leo Oktoba 29, 2024 jijini Dodoma wakati akifungua Kikao cha Makatibu Wakuu cha Maandalizi ya Mkutano wa 29 wa Nchi Wanachama wa Umoja wa Mataifa wa Mabadiliko ya Tabianchi (COP29) unaotarajiwa kufanyika kuanzia Novemba 11 hadi 22, 2024 Baku, Azerbaijan.
Mhandisi Luhemeja amesema kuwa pamoja na juhudi za Serikali katika kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi changamoto hiyo bado ni kubwa hivyo, amezitaka wizara, taasisi na wadau kuifanya ajenda ya mazingira kuwa ni moja ya vipaumbele vyake.
Ametoa wito kwa wajumbe watakaoshiriki katika mkutano huo watambue kuwa wanakwenda kutafuta fursa hususan za kifedha kwa ajili kuwezesha nchi kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi.
“Kila mmoja wetu aguswe na suala la mazingira, tunapokwenda kushiriki COP29 tusiende kimazoea, maazimio tunayoyafikia yasiishie kwenye makaratasi tuyawasilishe kwenye mkutano na yaje na matokeo, tunataka mkutano huu ulete mabadiliko katika nchi yetu,” amesisitiza.
Aidha, Mhandisi Luhemeja amesema kuwa lengo la Ofisi ya Makamu wa Rais ni kuhakikisha kila wizara, taasisi na wadau wanawekeza katika sekta ya mazingira kwani inagusa maeneo yote.
Akifafanua zaidi, Katibu Mkuu Luhemeja amesema kuwa mazingira yanagusa maisha ya mwanadamu kwa asilimia kubwa katika sekta mbalimbali kupitia Malengo ya Milenia ikiwemo kuondoa umaskini na njaa.
Ili kuepukana na njaa, ametoa wito kwa jamii kushiriki kikamilifu katika utunzaji wa mazingira hususan kwenye vyanzo vya maji kwani maji ni uhai wa mwanadamu.
Kwa upande wa nishati safi ya kupikia, Mhandisi Luhemeja amesema kuwa ajenda hiyo ni mbadala wa mapambano dhidi ya ukataji wa miti huku akiwahimiza wananchi kuacha matumizi ya kuni na mkaa ambayo yanachangia uharibifu wa mazingira.
Amesema nishati safi ya kupikia si gesi pekee bali inahusisha mbinu mbalimbali huku akipongeza Wakala wa Nishati Vijijini (REA) kwa kuwa na mikakati ya kuendeleza nishati mbalimbali zikiwemo umeme, hatua inasaidia kupunguza ukataji wa miti.
Kwa upande wake Mshauri wa Rais katika Masuala ya Mabadiliko ya Tabianchi na Mazingira Dkt. Richard Muyungi amesema washiriki wa CO29 watakuwa na kazi ya kuhakikisha ajenda za nchi zinakubalika na kupita.
Amesema mabadiliko ya tabianchi ni fursa ambayo Tanzania inapaswa kuitumia ipasavyo katika kufanya majadiliano na nchi zitakazoshiriki katika mkutano huo kupitia matukio 299.
Dkt. Muyungi ameeleza kuwa ushirikiano uliopo baina ya nchi na wadau wa maendeleo duniani ambao unapaswa kuwa ni mojawapo ya hatua zitasaidia katika maendeleo ya nchi.
“Unapokwenda kwenye COP hivi sasa unakuta watu wengi kama private sectors (sekta binafsi), kampuni, NGOs, ili sasa kutafuta ushirikiano wa kupunguza gesijto na hili sasa sio suala la Serikali tu ni suala la uashirikiano
na wadau,” amesisitiza.