Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan akihutubia viongozi mbalimbali kabla ya kufungua Mkutano wa 11 wa Merck Foundation Africa Asia Luminary katika hoteli ya Johari Rotana Jijini Dar es Salaam tarehe 29 Oktoba, 2024. Mkutano huo ni Kongamano la kielimu linalofanyika kila mwaka ili kuchangia maendeleo ya kijamii na kiuchumi katika Bara la Afrika na Asia.
…………..
Serikali ya Tanzania imeonyesha dhamira yake thabiti katika kuboresha sekta za afya na elimu, ambapo Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ameweka wazi jinsi uwekezaji wa serikali ulivyoleta mafanikio makubwa tangu mwaka 2021 hadi 2023. Katika hotuba yake leo, Oktoba 29, 2024, wakati wa ufunguzi wa mkutano wa 11 wa Merck Foundation, Rais Samia alieleza jinsi serikali yake ilivyoimarisha sekta hizo, hatua zinazowalenga hasa wanawake na watoto.
Mkutano huo wa Merck Foundation, unaofanyika kwa siku mbili Jijini Dar es Salaam, unalenga kujadili changamoto za afya na elimu zinazolikumba Bara la Afrika na Asia, ukiwa na kauli mbiu ya kutafuta suluhu endelevu kwa matatizo yanayowakabili wanawake na wasichana katika nyanja hizo.
“Tangu nikiwa Makamu wa Rais, nililenga kuboresha afya ya mama na mtoto, na leo tunajivunia kuona mafanikio yaliyopatikana. Tumejenga hospitali za wilaya 127 na vituo vya afya 367 kote nchini, hatua ambayo imepunguza vifo vya uzazi kwa zaidi ya asilimia 80,” alisema Rais Samia.
Aidha, Rais Dkt. Samia ametoa wito kwa Wenza hao viongozi kutumia ushawishi walionao kuunga mkono ajenda ya matumizi ya Nishati Safi ya kupikia katika nchi zao.
Katika mkutano huo, Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake, na Makundi Maalum, Dkt. Dorothy Gwajima, alisisitiza umuhimu wa mijadala ya kisayansi kwa ajili ya kukabiliana na magonjwa yanayowakumba wanawake, kama saratani na ugonjwa wa sukari, akisema kuwa Tanzania imepiga hatua kubwa katika kuweka sera zinazounga mkono usawa wa kijinsia na kuimarisha uwezeshaji wa wanawake.
Naye Mwenyekiti wa Bodi ya Merck Foundation, Profesa Frank Stangenberg-Haverkamp, aliwataka viongozi na wadau kuendeleza juhudi za kuondoa unyanyapaa unaokabili magonjwa ya afya ya uzazi na kuongeza fursa za elimu kwa wasichana. Mkutano huo umehudhuriwa na washiriki zaidi ya 700, wakiwemo wake wa marais kutoka nchi 15, na unatoa fursa kwa nchi wanachama kubadilishana uzoefu na mikakati bora.
Kwa kuendelea kushirikiana na taasisi kama Merck, Tanzania inaonyesha kuwa inajiimarisha katika kutatua changamoto za kijamii kwa kuwekeza katika sekta muhimu, hasa zinazolenga afya ya uzazi na elimu ya wasichana.
Mwenza wa Muasisi wa Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar Hayati Abeid Amani Karume mama Fatma Karume kushoto na Siti Mwinyi Mwenza wa Rais Mstaafu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Hayati Ali Hassan Mwinyi wakiwa katika ufunguzi wa Mkutano wa 11 wa Merck Foundation Africa Asia Luminary uliofanyika katika hoteli ya Johari Rotana Jijini Dar es Salaam tarehe 29 Oktoba, 2024.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan akisalimiana na Wenza wa Wakuu wa nchi mbalimbali Barani Afrika mara baada ya ufunguzi wa Mkutano wa 11 wa Merck Foundation Africa Asia Luminary uliofanyika katika hoteli ya Johari Rotana Jijini Dar es Salaam tarehe 29 Oktoba, 2024.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan akiwa kwenye picha ya pamoja na Wenza wa Wakuu wa nchi mbalimbali Barani Afrika mara baada ya ufunguzi wa Mkutano wa 11 wa Merck Foundation Africa Asia Luminary uliofanyika katika hoteli ya Johari Rotana Jijini Dar es Salaam tarehe 29 Oktoba, 2024. Aidha, Rais Dkt. Samia ametoa wito kwa Wenza hao viongozi kutumia ushawishi walionao kuunga mkono ajenda ya matumizi ya Nishati Safi ya kupikia katika nchi zao.