Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu leo (Jumanne, Oktoba 29, 2024) imetangaza Awamu ya Nne (Batch Four) yenye wanafunzi 9,068 wa shahada ya awali (Bachelor Degrees) na stashahda (Diploma) waliopangiwa mikopo yenye thamani TZS 27.52 bilioni kwa mwaka wa masomo 2024/2025.
Wanafunzi 4,400 wa mwaka wa kwanza waliodahiliwa katika taasisi mbalimbali za elimu ya juu zilizopo nchini kwa ajili ya masomo ya shahada za awali na wamepangiwa mikopo yenye thamani ya TZS 13.74 bilioni. Awamu hii pia imewajumuisha wanafunzi 2,646 wa shahada ya awali wanaoendelea na masomo ambao wamepangiwa mikopo kwa mara ya kwanza (first-time continuing) yenye thamani ya TZS 8.37 bilioni.
Katika awamu ya nne iliyotangazwa leo, wamo pia wanafunzi wapya 2,022 wa stashahada wa mwaka wa kwanza ambao wamepangiwa mikopo yenye thamani ya TZS 5.41 bilioni. Wanafunzi hawa wamedahiliwa katika programu za kipaumbele katika vyuo mbalimbali vya kati hapa nchini.
Ruzuku ya ‘Samia Scholarship’
Mpaka sasa, jumla ya TZS 3.14 bilioni zimetolewa kwa ajili ya ruzuku kwa wanafunzi 625; (588 awamu ya kwanza, 11 awamu ya pili na 26 awamu ya tatu) kwa wanafunzi wa shahada ya awali, mwaka wa kwanza wanaonufaika na ‘Samia Scholarship’ kwa mwaka wa masomo 2024/2025 katika fani za Sayansi, Teknolojia, Uhandisi, Hisabati na Tiba.
Kufunguliwa kwa Dirisha la Rufaa 2024/2025
Kupitia taarifa hii, wanafunzi walioomba mikopo kwa mwaka wa masomo 2024/2025 lakini hawakuridhika na viwango vya awali walivyopangiwa au hawajapangiwa mikopo, wanashauriwa kukata rufaa ndani ya siku saba kuanzia Jumatatu, Novemba 4 hadi Jumapili, Novemba 10, 2024.
The post 9068 wapangiwa mikopo ya TZS 27.5 Bilioni awamu ya Nne first appeared on Millard Ayo.