Na Sophia Kingimali,Dar es salaam.
SERIKALI imewataka Wabunifu wa Majengo na Wakadiriaji Majenzi Nchini kufanya kazi kwa uzalendo katika utekelezaji wa miradi wanayopewa kwa wakati na kwa ubora ili kujenga uaminifu na kuaminiwa na serikali na sekta binafsi.
Wito huo umetolewa leo Octoba 29,2024 Jijini Dar es salaam na Mkuu wa Wilaya ya Ilala Edward Mpogolo wakati akimuakilisha Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati Dotto Biteko katika mkutano wa Tano wa Bodi ya wabunifu na Wakasiriaji Majenzi uliyofanyika katika ukumbi wa mikutano wa kimataifa wa Julius Nyerere sambamba na mahafali ya kwanza ya wahitimu wa mafunzo ya taaluma ya wabunifu Majengo na wadiriaji Majenzi ,ambapo zaidi ya wahitimu 130 wamehitimu.
Mpogolo amesema kuwa baadhi ya wataalamu wa ubunifu wa Majengo na ukadiriaji Majenzi wamekua wakiangalia maisha yao binafsi kwa ajili ya kujipatia fedha huku suala la weledi likiwa kimewekwa pembeni hali ambayo inasababisha Majengo kuwa chini ya kiwango.
Aidha amesema kwasasa serikali ipo kwenye mchakato wa kufanyia maboresho sera ya ujenzi ili kutengeneza Sheria ya ujenzi lengo likiwa kuhakikisha Sekta ya ujenzi inafanikiwa kupitia wataalam mbalimbali wa ndani wa sekta hiyo wakiwemo wabunifu wa Majengo na Wakadiriaji Majenzi.
“Jitihada zinazopatikana katika sekta ya ujenzi zinatokana na nyinyi wataalamu wa ubunifu wa Majengo na ukadiriaji Majenzi,ukiona mafanikio yaliyopo kwa sasa yanatokana na nyinyi,hivyo nawaomba sana muwe Wazalendo” amesema Mpogolo.
Kwa upande wake mwakilishi wa Katibu Mkuu Wizara ya Ujenzi Dkt Daudi Kondoro ambaye pia ni Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa Majengo Tanzania( TBA) amesema kuwa watendaji wa Wizara wataendelea kusimamia sekta ya wataalamu wa ubunifu wa Majengo na Wakadiriaji Majenzi ili waweze kua na weledi katika kazi zao kwa maslahi ya nchi
“Wizara ya ujenzi itatenga fedha kwa ajili ya kuendelea kutoa mafunzo kwa wataalamu 180 Kila Mwaka ambao wanahusika na bunifu wa Majengo na ukadiriaji Majenzi,ili waweze kuwa na uelewa Mzuri katika taaluma yao” amesema Dkt.Kondoro.
Naye, Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Bodi wa wabunifu wa Majengo na Wakadiriaji majenzi (AQRB) Dkt Ludigija Bulamile amesema kuwa kwa sasa Bodi hiyo imesajili 1586 ambapo kati yao 33 ni wageni kutoka nje ya nchi.
“Kuna ongezeko la wabunifu majengo wenye ustadi na ubunifu mkubwa katika kuleta matokeo chanya katika Taifa letu lakini pia tumekuwa na juhudi katika kuwatafuta wahitimu na kuwapatia mafunzo na katika hili tumefanikiwa kuwapatia elimu watihimu katika sekta hii”,Amesema.