Wananchi wa Botswana leo tarehe 30 Oktoba 2024 wamepiga kura kuchagua wabunge watakaounda Bunge la 13 la nchi hiyo na wenyeviti wa Serikali za mitaa ambao wataongoza nchi hiyo kwa kipindi cha miaka mitano ijayo.
Mkuu wa Misheni ya Uangalizi wa Uchaguzi ya Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC-SEOM) Mhe. Mizengo Pinda na timu yake wametembelea vituo vitatu vya kupigia kura katika jiji la Gaborone na vituo viwili katika kijiji cha Mochudi kujionea hali ya upigaji kura inavyoendelea.
Jumla ya Viti 61 vya ubunge na vinagombewa na wagombea kutoka vyama vinne vya siasa vya Botswana Democratic Party (BDP); Umbrella for Democratic Change (UDC); Botswana Congress Party (BCP) na Botswana Patriotic Front (BPF) ambapo Viti 609 vya mabaraza ya Serikali za mitaa vinagombewa na vyama mbalimbali vya siasa na wagombea binafsi ambao wamekidhi vigezo vilivyowekwa na Tume Huru ya Uchaguzi nchini humo (IEC).
Uchaguzi mkuu wa Botswana umeshuhudiwa na waangalizi wa kimataifa kutoka wa Misheni za Umoja wa Afrika (AUEOM) iliyoongozwa na Rais wa Mstaafu wa Nigeria, Mhe. Goodluck Jonathan, Misheni ya Uangalizi wa Uchaguzi wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC-SEOM) iliyoongozwa na Waziri Mkuu wa Zamani wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Mizengo Pinda, Misheni ya Uangalizi wa Uchaguzi ya Jumuiya ya Madola iliyoongozwa na Mhe. Gideon Moi, na Jukwaa la Tume za Uchaguzi kutoka nchi za SADC lililoongozwa na Mwenyekiti wa Tume Huru ya Uchaguzi Tanzania (INEC), Mhe. Jaji Jacob Mwambegele.
Sambamba na hilo, uchaguzi huo umeshuhudiwa na Ubalozi wa Marekani, Japan, Indonesia, Namibia na waangilizi kutoka katika taasisi mbalimbali zinazoshughulikia masuala ya siasa kutoka nchini humo.
Misheni hizo zimewapongeza wananchi wa Botswana kwa kuendesha shughuli za uchaguzi kwa amani na usalama katika siku ya uchaguzi mkuu ambapo waangalizi hao wameshuhudia idadi kubwa ya wapiga kura ikiwa imejitokeza kupiga kura katika hali ya amani na usalama katika jiji la Gaborone.
Kwa mujibu wa utaratibu wa uchaguzi nchini humo chama kitakachopata zaidi ya viti 31 vya Bunge ndicho kitakachotoa Rais ambaye ataunda Serikali itakayoongoza nchi hiyo kwa kipindi cha miaka mitano ijayo.