NA EMMANUEL MBATILO, MICHUZI TV
BENKI Kuu ya Tanzania (BoT) imesema zoezi la kubadilisha noti za zamani litaanza rasmi Januari 6, mwakani na kwa kipindi cha miezi mitatu hadi Aprili 5, hivyo basi Watanzania wametakiwa kuziwasilisha fedha hizo benki.
Akizungumza na waandishi wa habari leo Oktoba 31, 2024 Jijini Dar es Salaam, Kaimu Mkurugenzi Usimamizi wa Sarafu BoT, Ilulu Ilulu amesema zoezi la ubadilishwaji litafanyika ofisi zote za Benki Kuu na benki zote za biashara nchini kwa kupatiwa malipo yenye thamani sawasawa na kiasi kilichowasilishwa.
Aidha amewataka Watanzania wahakikishe wanakwenda kubadilisha noti tu zilizo halali zenye alama za usalama na faida ya kufanya hivyo ni kupata thamani ambayo walidhani imepotea na baada ya miezi hiyo kupita watazifuta kabisa.
“Inapotokea kusitisha uhalali wa noti fulani wananchi hupewa muda maalumu wa kuzibadilisha noti hizo kabla ya kusitisha uhalali huo , hupewa fursa ya kubadilisha noti husika kwa kupewa kiwango kilekile”. Amesema
Pamoja na hayo amewataka Watanzania kuacha kuuza na kukununua noti chakavu mitaani kwani ni kosa kisheria na kinachofanyika ni utapeli.
Amesema wananchi wanatakiwa kwenda kubadilisha noti hizo katika Benki za Biashara nchini kwani kuna madirisha maalumu ya kubadilishia fedha hizo.
“Suala la kununua na kuuza sarafu halipo kisheria ni kosa kwa sababu kinachofanyika hapo ni kumtapeli mwenzako kutokana na kutokuwa na taarifa, BoT imetoa fursa kwa Benk izote za Biashara nchini kuwa na dirisha la kubadilisha noti chakavu,”alisema.
Kutokana na hilo amewataka wananchi kwenda wenyewe kubadilisha fedha hizo katika madirisha yaliyofunguliwa katika benki zote za biashara kunufaika na huduma hiyo.