Na Mwandishi Wetu, Michuzi Tv
KAMATI ya Kudumu ya Bunge ya Viwanda, Biashara, Kilimo na Mifugo imeridhishwa na kasi ya ujenzi wa mtambo mpya wa mabati ya rangi wa ALAF Limited na kuitaka serikali iweke mazingira mazuri ya uzalishaji na biashara kwa ujumla ili kiwanda hicho kiweze kuzalisha zaidi na kutengeneza faida.
Kauli hiyo imetolewa na Mwenyekiti wake, Deo Mwanyika ambaye kwa niaba ya kamati ameipongeza ALAF kwa uwekezaji huo mkubwa wa kiwanda kipya cha mabati ya rangi ambacho kinatarajiwa kuanza uzalishaji mwezi ujao.
“Tumekuja kutembelea kiwanda na kujionea maendeleo ya mtambo huu mpya wa rangi tumefarajika kuona kwamba hivi karibuni tu uzalishaji utaanza, sisi kama kamati tutachukua maoni yenu kama vile kodi zenye kero na uwanja usiokuwa sawa wa biashara,” amesema.
Amesema mtambo mpya wa rangi utahakikisha ubora zaidi, ajira zaidi kwa watanzania na kwamba hakutakuwa na uingizaji wa mabati ya aina hii kutoka nje kwani uzalishaji utatosheleza mahitaji ya nchi nzima.
“Tumefurahi pia kusikia kuwa mtambo huu mpya utaendeshwa na watanzania ambapo tayari mainjinia 30 vijana wamepokea mafunzo ya kina nje ya nchi,” amesema.
Kwa mujibu Mwanyika, kamati imekubaliana na ALAF kuwa watafanya kikao kingine cha pamoja Dodoma ili ALAF wawasilishe masuala yote na kamati ijadili kwa kina na kuyaelewa ili wayawasilishe serikalini kwa usahihi.
“Leo tumekuja kufanya ziara tu hatuwezi kujadiliana na kumaliza kila kitu leo tunahitaji kukaa tena kwa pamoja tuyaangalie haya masuala vizuri,” ameeleza.
Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara Exaud Kigahe ameipongeza ALAF kwa uwekezaji huo mkubwa na kusisitiza kuwa serikali itafanya kila jitihada kuhakikisha inaweka mazingira bora ya biashara na kwamba mtambo mpya wa ALAF wa rangi unazalisha kwa faida.
“ALAF inazalisha mabati yenye ubora mkubwa sana na sisi kama serikali tunataka watanzania waweze kupata biadhaa zenye ubora kwa maana hiyo hatuna budi kuhakikisha vikwazo vilivyopo kwa sasa vinaondoka ili waweze kufanya biashara kwa ufanisi,” ameeleza na kuongeza kuwa watakaa pamoja na uongozi wa ALAF ili kutatua kero zilizopo
Naye, Afisa Mtendaji Mkuu wa ALAF Limited, Ashish Mistry ameishukuru Kamati hiyo kwa kutenga muda wa kutembelea ALAF na kuwahakikishia kuwa kiwanda kipya cha mabati ya rangi kitaanza uzalishaji mwezi ujao.
“Tunawahakikishia ubora wa hali ya juu wa mtambo huu ambao utakuwa bora kabisa Afrika na utazalisha zaidi ya mahitaji ya Tanzania,” amesema.
Meneja Uhusiano na Mawasiano wa ALAF, Hawa Bayumi ametoa wito kwa Watanzania wapende vya nyumbani na wajiandae kwa ubora wa hali ya juu huku akisisitiza kuwa kwa msaada wa kamati hiyo ya bunge, wanaamini serikali itatatua kero zote ambazo zinaathiri uzalishaji kwa sasa.
“Tunachohitaji kama ALAF ni uwanja sawa wa kufanyia biashara na mazingira bora, amesema na kuongeza kuwa kiwanda kipya kitakuwa na uwezo wa kuzalisha tani 75,000 kwa mwaka ambazo ni zaidi ya mahitaji ya Tanzania.
ALAF Limited ni kampuni inayoongoza nchini Tanzania kwa kutengeneza mabati ya kuezekea nyumba. Ni kampuni iliyoanzishwa mwaka 1960, na inaendelea kuwa mdau muhimu katika maendeleo ya sekta ya ujenzi nchini.
ALAF imeunganisha kikamilifu operesheni, si tu kwa kutengeneza mabati, lakini pia kwa kuzalisha vifaa vinavyotumika katika shughuli mbalimbali za uezekaji wa nyumba. ALAF Limited hutengeneza vifaa mbalimbali vya metali kwa matumizi mbalimbali ya uezekaji wa nyumba.
Wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Viwanda, Biashara, Kilimo na Mifugo wakitembelea Kiwanda cha ALAF Limited Jijini Dar es Salaam kukagua maendeleo ya kiwanda kipya cha mabati ya rangi na pia kuangalia namna ya kuishauri serikali x changamoto zinazoathiri uzalishaji kiwandani hapo kwa sasa.