Na Karama Kenyunko Michuzi Tv
MOHAMED Omar (64) na dada yake Nargis Omary (70) wamefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu wakilabiliwa na mashtaka mawili likiwemo la kughushi wosia.
Hata hivyo ni mshtakiwa Mohamed tu ndiye aliyesomewa mashtaka huku mahakama ikielezwa kuwa mshtakiwa Nargis ameruka dhamana ya polisi.
Katika hati ya mashtaka iliyosomwa mahakamani hapo na wakili wa serikali Neema Moshi mbele ya Hakimu Mkazi Mfawidhi, Franco Kiswaga imedai washtakiwa walitenda makosa hayo Kati ya Julai 29,1997 na Oktoba 28,1998 ndani ya jiji na mkoa wa Dar es Slaam. Dar es Salaam
Inadaiwa siku hiyo washtakiwa kwa pamoja wallghushi wosia kwa dhumuni la kuonyesha kuwa ni nyaraka halali ya wosia uliotolewa na marehemu Rukia Ahmed Omar maarufu kama Rukia Sheikh huku wakijua kuwa siyo kweli.
Katika shtaka la pili inadaiwa siku na mahali hapo washtakiwa waliwasilisha nyaraka ya uongo mahakamani ikionyesha kuwa marehemu Rukia alitoa nyumba plot namba 35 iliyopo Kariakoo jijini Dar es Salaam kwa mtu aitwaye Nargis Omar na nyumba ploti namba 60 iliyopo Magomeni jijini Dar es Salaam kwa mtu aitwaye Mohamed Omary huku wakijua kuwa siyo kweli.
Hata hivyo mshtakiwa Mohamed amekana kutenda kosa hilo na yuko nje kwa dhamana baada ya kutimiza masharti ya mahakama yaliyomtaka kuwa na wadhamini wawili watakaosaini bondi ya Sh. Milioni tano kila mmoja, haruhusiwi kusafiri nje ya nchi bila kupata kibali cha mahakama.
Kwa mujibu wa upande wa mashtaka upelelezi katika kesi hiyo bado haujakamilika, kesi imeahirishwa hadi Desemba 4,2024.