Kwa upande mwingine, Diwani wa Kata ya Masanga, Mhe. Enock Reuben, amebainisha kuwa kata hiyo imekusanya zaidi ya Shilingi Milioni 14 katika robo hii ya kwanza ya mwaka 2024/2025. Hata hivyo, ameeleza kwamba mradi wa maji safi wa Masanga-Ndololeji, uliotakiwa kukamilika mwezi Agosti 2024, umechelewa kukamilika na hivyo kuathiri huduma za maji kwa wananchi wa kata hiyo.
Taarifa za Kata ya Ngofila, zilizowasilishwa na Diwani Mhe. Nestori Ngude, zilionyesha kuwa kata hiyo inakabiliwa na changamoto za upungufu wa vyumba vya madarasa katika baadhi ya shule za msingi, uhaba wa madawati, na matatizo ya miundombinu ya vyoo. Aidha, mradi wa maji safi na salama unakumbwa na ucheleweshaji,na ujenzi wa zahanati ya Inolelo bado haujakamilika.
Wakati huo, Diwani wa Kata ya Kiloleli, Mhe. Edward Manyama, amezungumzia umuhimu wa kufanya ukarabati wa mapema wa barabara, akisisitiza kwamba hatua hiyo itasaidia kupitisha masanduku ya kupigia kura kwa usalama kipindi cha uchaguzi, hasa wakati wa mvua.
Akijibu hoja hizo, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Kishapu, Bw. Emmanuel Johnson, amewataka wakuu wa idara kuwa makini katika kufuatilia changamoto zilizobainishwa katika taarifa za kata na madiwani ili ziweze kushughulikiwa haraka.
Ametoa wito kwa madiwani na wananchi kuipa kipaumbele zahanati, na kuahidi kuwa serikali itaendelea kutenga fedha kwa ajili ya ukarabati wa miundombinu ya barabara.
“Kwa bahati nzuri, tunaanza mwaka wa fedha, hivyo niwashauri waheshimiwa madiwani na wananchi tuzipe zahanati zetu kipaumbele na kuzitengea fedha ili kumaliza ukarabati haraka iwezekanavyo, kama vile zahanati za Bubiki na Inolelo kata ya Ngofila,” amesema Bw. Johnson.
Ameongeza kuwa Serikali ya Awamu ya Sita imeongeza bajeti kwa ajili ya ukarabati wa miundombinu ya barabara, ambapo baadhi zitajengwa kwa kiwango cha lami, huku pia wakandarasi wakianza kazi hivi karibuni.
Katibu wa CCM Wilaya ya Kishapu, Peter Mashenji, amewataka watendaji wa halmashauri hiyo kuchukua hatua za haraka katika kushughulikia changamoto hizo ili kujibu hoja za wananchi na kuhakikisha maendeleo ya kata yanapata kasi ya utekelezaji.
Katika ujumla, kikao hicho kimejikita katika kufuatilia maendeleo ya miradi na changamoto zinazokabili maeneo mbalimbali ya Wilaya ya Kishapu, huku viongozi wakihimiza ushirikiano wa pamoja kati ya serikali, madiwani, na wananchi ili kufanikisha utekelezaji wa miradi ya maendeleo na kuboresha huduma za kijamii.