KATIKA kuongeza uelewa wa
masuala ya fedha kwa maendeleo na ukuaji kiuchumi kwa Mtanzania mmoja
mmoja na Taifa kwa ujumla, Benki ya NMB imezindua Programu Endelevu ya
Elimu ya Fedha iitwayo NMB Nondo za Pesa, itakayotolewa kupitia vyombo
habari, mitandao ya kijamii na makongamano.
NMB Nondo za Pesa
imezinduliwa na Afisa Mkuu wa Wateja Binafsi na Biashara wa NMB, Filbert
Mponzi jijini Dar es Salaam Jumatatu ya Novemba 4, ambapo alisema
walisema walengwa wa programu hiyo Watanzania wote, lakini kwa upekee,
itakuwa na vipengele maalumu vinavyowagusa Vijana na Wanawake.
Mponzi,
ambaye alimwakilisha Afisa Mtendaji Mkuu wa NMB, Bi. Ruth Zaipuna,
alisema kupitia Nondo za Pesa, benki yake itakuwa inatoa elimu kwenye
mada muhimu zote kuhusiana na fedha, ikiwamo namna ya kupanga bajeti,
kuweka akiba, uwekezaji, mikopo, bima na mipango mingine ya kifedha.
“Lengo
la kusambaza Elimu ya Fedha kwa umma wa Watanzania ni umuhimu wake
mkubwa kwa jamii, kukosa elimu hiyo kumewaingiza wengi kwenye changamoto
za kimaisha, kiuchumi, kielimu, kiafya. Mikopo kandamizi ‘kausha damu,’
ni zao la ukosefu wa elimu ya fedha, ambayo sisi Taasisi za Fedha ni
wajibu wetu.
“Walengwa ni Watanzania wote, ila kwa kipekee
tutayagusa makundi ya vijana ambalo linajumuisha asilimia 66 ya
Watanzania na wanawake. Kwanini Vijana, ni kwa sababu ni kundi lenye
fursa kubwa ya kiuchumi, ingawa tayari tuna jukwaa lao maalum la
GOnaNMB, lakini bado tunalenga kuwapa vijana mbinu bora za kifedha.
“Wanawake
watafikiwa zaidi na NMB Nondo za Pesa, kwa sababu hawa ni nguvu kuu
katika uchumi wa familia na jamii. Pia, wao tunalo jukwaa lao maalum la
JASIRI ambalo linawawezesha kwa kuwapa maarifa ya kifedha, akiba, na
mikopo salama inayosaidia kuanzisha au kuendeleza biashara zao,”
alifafanua Mponzi.
Uzinduzi huo uliohudhuriwa na makundi
mbalimbali ya vijana na wanawake, Wanafunzi wa Elimu ya Juu,
wajasiliamali, bodaboda, mama na baba lishe, ulienda sambamba na
uzinduzi wa kipindi cha runinga kiitwacho The Junction, kitachoruka mara
moja kwa mwezi na kutoa elimu ya fedha kwa Watanzania wote.
“Kulingana
na takwimu ya Finscope ya Mwaka 2023, mtu mmoja kati ya 10 wenye
akaunti za kibenki ndio wanaokopa benki, hii ikatusukuma NMB kuona
umuhimu wa Watanzania hususani Vijana na Wanawake, wakajua huduma zetu
mahususi ambazo wanaweza kunufaika nazo kwa kuingia tu kwenye mfumo
ramsi.
“Nondo za Pesa ni muendelezo wa huduma rafiki za NMB kwa
Watanzania, zikiwemo NMB Kikundi Akaunti (ambayo ni maalum kwa vikundi
vya kijamii), NMB Jiwekee inayomuwezesha mteja wetu aliye nje ya mifumo
rasmi ya ajira kujiwekea akiba, pia tunayo Mshiko Fasta, mkopo
usiohitaji dhamana wala ujazazi fomu,” aliongeza Mponzi.
Alitaja
huduma zinginea rafiki kwa Watanzania kuwa ni NMB Pesa akaunti isiyo na
makato ya mwezi inayofunguliwa kwa Sh. 1,000, Spend to Save inayokupa
uhuru wa kujiwekea akiba kulingana na matumizi yako yanayopitia kwenye
akaunti yako asilimia utakazojichagulia.
“NMB ni kinara wa
mapinduzi ya huduma na Nondo za Pesa itaenda kumnufaisha kila mmoja
popote alipo kupitia kipindi cha televisheni, radio, mitandao ya
kijamii, makongamano, meseji za dondoo za fedha kwa wateja wetu,
madarasa ya elimu za kifedha, kliniki za elimu za fedha kwenye matawi
yetu,” alisema Mponzi.
Wakizungumza baada ya uzinduzi huo, Frank
Silvester Mrope ambaye ni Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Madereva na
Wamiliki wa Pikipiki na Bajaji (CMPD Wilaya ya Kigamboni), alisema
amefurahia ujio wa NMB Nondo za Pesa ili kuwajengea uelewa na uwezo
wasafirishaji wa chama chake ambao ni wanufaika vinara benki hiyo.
“NMB
wamekuwa wadau wetu wakubwa, wametukopesha pesa, lakini pia vyombo vya
usafiri kama pikipiki na bajaj, kwa hiyo sisi ni wanufaika wakubwa wa
huduma zao na walichofanya hapa ni kutuongezea elimu zaidi za utafutaji
na uwekaji akiba kwa faida yetu na vizazi vyetu.
“Wito wangu kwa
bodaboda na bajaj ambao wako nje ya vyama, wajitokeze kujisajili ili
kuingia kwenye mifumo rasmi ya kibenki, waweze kukopesheka, kwa sababu
ni ngumu kwao kupata fursa wakiwa nje ya mifumo” alisema Mrope.
Naye
Mussa Julius, ambaye ni Afisa Habari wa CMPD Wilaya ya Kinondoni,
aliwapongeza NMB kwa kuwajali na kuwathamini waendeshaji wa bodaboda na
bajaj Dar es Salaam kwa kuja na program hiyo, huku akiitaka kuwafuata
madereva vijiweni na mitaani kuwapa elimu hiyo, kwani wengi wao hawana
elimu ya fedha.
“Tumeipokea NMB Nondo za Pesa, tunaiomba NMB
iandae mpango mkakati wa kuwafikia madereva wetu, ambao hawana elimu ya
fedha. Tumefikia hatua ya kutokuwa na akiba kubwa, licha ya kuhudumu kwa
muda mrefu katika sekta ya usafirishaji, kwahiyo hii ‘project’
tunaamini itakuwa mwarobaini,” alibainisha
Kwa upande wake, Ruth
Lema wa Soko la Wajasiliamali la Mbezi kwa Beda, jirani na Stendi Kuu ya
Mabasi ya Magufuli, alisema uzinduzi wa NMB Nondo za Pesa umekuja na
manufaa makubwa kwao kwani wamejifunza vitu vingi ikiwemo fursa za
ukopaji, uwekezaji, bima na masuala mazima ya elimu ya fedha.
“Tumefurahia
uzinduzi huu, umetuongezea vitu vingi ikiwemo namna mbalimbali za
kukopa, matumizi sahihi na umuhimu wa urejeshaji wa mikopo na fursa
zingine nyingi kwa vijana na wanawake. Wito wangu kwa wajasi;iamali wote
kujiunga na vikundi vya kijamii na kunufaika pamoja na huduma za NMB,”
alisema Bi. Ruth.