Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko amewataka wadau wa sekta ya uziduaji kubainisha fursa na changamoto zilizopo katika sekta hiyo, kujadiliana kwa uwazi na kuambizana ukweli kuhusu hali halisi katika sekta hiyo.
Dkt. Biteko ameyasema hayo Novemba 5, 2024 Jijini Dodoma wakati wa uzinduzi wa Jukwaa la Uziduaji kwa Mwaka 2024 lenye kauli mbiu “Sekta ya Uziduaji, Maendeleo Endelevu na Mhamo wa Nishati Tanzania”.
“Semeni kwa uwazi na kuambizana ukweli ili kusukuma maendeleo kwa pamoja, mngejua kuhusu matishio ya dunia na siasa za ulimwengu, dunia inapita katika misukosuko mingi ikiwemo mabadiliko ya tabia nchi na matokeo yake ni ongezeko la idadi ya matetemeko ya ardhi katika maeneo mbalimbali duniani hivyo katika majadiliano yenu, angalieni michango ya nchi, visababishi na mahitaji yake,”
Ametoa mfano kuwa tafiti zinaonesha kumekuwa na ongezeko la idadi ya matetemeko ya ardhi kutoka tisa mwaka 1950 hadi matetemeko 51 miaka ya 1970 idadi ambayo imeongezeka kufikia 150 miaka ya 1990 jambo ambalo amelitaka Jukwaa la Uziduaji kujadiliana kwa kina kuhusu mwelekeo wa halisi wa maendeleo ya Bara la Afrika kwa miaka ijayo.
“Wakati dunia ikiwa katika hatari kubwa inayotokana na matumizi ya nishati isiyo safi na salama, tujadili mchango wa mtu na nchi mojamoja ili kufikia maamuzi sahihi yatakayowezesha kuleta maendeleo, kila mtu na mchango wake kulingana na hali yake mfano nchi kama Marekani mtu mmoja kwa mwaka anatumia wastani wa mapipa 22 ya mafuta huku wastani kwa nchi za Afrika ni matumizi ya pipa moja kwa mwaka” amesema Dkt. Biteko.
Amesema kuwa Sekta ya Uziduaji kwa ukubwa wake inajumuisha rasilimali za madini, mafuta na gesi ambazo ni muhimu katika maendeleo ya Taifa. Kwa kuzingatia umuhimu wake Dira ya Maendeleo ya Taifa ya mwaka 2025 iliainisha kuongeza kasi ya ukuaji wa sekta ya madini na kuongeza mchango wake katika Pato la Taifa kwa asilimia 10 hadi kufikia mwaka 2025 na kwa sasa kuna uhakika wa kufikia kiasi hicho.
Dkt. Biteko ametaja jitihada zinazofanywa na Serikali ambazo zimeendelea kuimarisha Sekta ya Nishati ikiwa ni pamoja na uwezo wa mitambo ya kufua umeme iliyounganishwa katika mfumo wa Gridi ya Taifa umeongezeka na kufikia Megawati 2,607.96 ikilinganishwa na Megawati 1,605.86 zilizokuwepo mwaka 2021 ikiwa ni ongezeko la asilimia 62 ambalo limetokana na kukamilika kwa miradi mbalimbali ya kuzalisha umeme nchini.
Aidha, ujenzi wa Bwawa la kuzalisha umeme la Julius Nyerere lenye uwezo wa kuzalisha Megawati 2,115 ambapo utekelezaji wake umefikia asilimia 99.21 na kwa sasa unazalisha MW 1,175.
Vilevile, Serikali imeendelea kuimarisha miundombinu ya kusafirisha umeme kwa kujenga njia mpya za kusafirisha umeme kufikia urefu wa kilomita 7,745.4 kutoka kilomita 6,111.27 zilizokuwepo mwaka 2021 ikiwa ni sawa na ongezeko la asilimia 26.7. Aidha, njia za kusambaza umeme zimeongezeka na kufikia urefu wa kilomita 187,817.3 ikilinganishwa na kilomita 153,988.49 za mwaka 2021, sawa na ongezeko la asilimia 21.9.
Naye, Waziri wa Madini, Mhe. Anthony Mavunde amesema kuwa Serikali imeendelea kuimarisha sekta ya madini ikiwa ni pamoja na kuongeza bajeti yake kwa mwaka hadi kufikia takribani shilingi bilioni 200 pamoja na kufanya utafiti wa kina wa madini na kuongoza vyema wachimbaji wadogo.
The post Wadau sekta ya uziduaji watakiwa kujadiliana, kuambizana ukweli first appeared on Millard Ayo.