Na Mwandishi Wetu, Katavi
Sheria ya Udhibiti wa Uzito wa Magari ya Jumuiya ya Afrika Mashariki ya mwaka 2016 na kanuni zake za mwaka 2018 zimeweka adhabu kali kwa magari yatakayokwepa kupima mizigo kwenye mizani zote nchini Tanzania.
Mwanasheria Mwandamizi wa Wakala ya Barabara Tanzania (TANROADS), Usaje Mwambene, amefafanua sheria hiyo hivi karibuni kwenye mafunzo ya watumishi wa mizani na wasafirishaji wa Kanda ya Magharibi.
Mafunzo hayo yaliyofanyika kwa siku nne mkoani Katavi yalijumuisha mikoa ya Rukwa, Tabora, Kigoma, na Katavi.
Usaje alisema sheria hiyo namba 7, kifungu cha 20(1), kimeorodhesha makosa na adhabu zake, likiwemo kosa la kukwepa kupima mizigo kwenye mizani, kusafirisha mzigo maalum bila kibali, au kukiuka masharti ya kibali hicho.
Mfano wa ukiukaji ni msafirishaji kuendesha gari nje ya muda ulioruhusiwa na kibali, kama vile kuendesha gari saa 2 au 3 usiku wakati kibali kinamtaka kusitisha safari saa 12 jioni.
Aidha, kifungu cha 20(2) cha sheria hii kinataja makosa kwa watumishi wa mizani kama vile kupima magari kwa kutumia mizani mbovu au kupokea rushwa, ikiwa ni fedha taslimu, maelekezo, au ahadi. Adhabu ya kosa hili ni faini ya dola za Kimarekani 15,000 au kifungo cha miaka mitatu au vyote kwa pamoja.
Hatahivyo, Usaje alisema lengo la sheria hii sio kukusanya faini bali ni kulinda barabara ili zidumu kwa muda uliokusudiwa.
“Kwa mfano, msafirishaji akimshawishi afisa wa mizani kumpitisha mzigo uliozidi kiwango kwa ahadi fulani, wote wawili wanakabiliwa na adhabu ikiwa mahakama itathibitisha makosa,” alisisitiza.
TANROADS kwa kushirikiana na Wizara ya Ujenzi wameanzisha programu za kutoa elimu kwa wasafirishaji na watumishi wa mizani kuhusu sheria hii ya mwaka 2016.
Pia TANROADS imepewa mamlaka, chini ya kifungu cha 22 cha sheria hiyo, kutoza faini ya dola 2,000 kwa makosa yanayojirudia nje ya mfumo wa kawaida wa mahakama.