NA WILLIUM PAUL, SAME.
WANANCHI wa Kata ya Kihurio wilayani Same Mkoani Kilimanjaro wameishukuru Serikali kuwapatia mradi mkubwa wa maji unaogharimu zaidi ya shilingi Bilioni 4.17 ambao utakuwa mwarobaini wa changamoto ya upatikanaji wa huduma ya maji safi na salama kwa wananchi zaidi ya 10,000 wa Kata hiyo.
Pili Salim, ni miongoni mwao Wakazi wa Kata hiyo ambaye alisema kukamilika kwa mradi huo kutakuwa suluhisho juu ya adha wanayoipata ya kulazimika kutembea umbali mrefu kutafuta huduma ya maji kwenye mito.
Kauli ya Wananchi hawa inaungwa mkono na Katibu wa Mbunge Jimbo la Same Mashariki, Semu Mmamba ambaye alisema huduma ya maji ni hitajio kubwa kwa Wananchi wa Kihurio, akiomba mkandarasi kuanza utekelezaji wa mradi huo kama mkataba unavyomtaka.
Akisoma taarifa ya utekelezaji wa mradi huo Meneja wa Wakala wa maji safi na usafi wa mazingira Vijijini (RUWASA) Mhandisi Abdallah Gendaeka amesema, mradi utatekelezwa kwa muda wa miaka miwili kuanzia Desemba 06 mwaka huu na kutarajiwa kukamilika Desemba 06 mwaka 2026.
Alisema kuwa kazi hiyo itafanywa na mkandarasi kutoka kampuni ya FESAM CONSTRUCTION LIMITED yenye makao makuu yake Jijini Dar es Salaam (mkandarasi mzawa).
Kwa upande wake, Meneja wa Ruwasa mkoa wa Kilimanjaro, Mhandisi Weransari Munisi, alisema kuwa kupaatika kwa fedha za mradi huo kunachagizwa na jitihada za Mbunge wa Jimbo la Same Mashariki Anne Kilango kwa lengo la kutaka Wananchi wake kuondokana na adha ya kutembea umbali mrefu kutafuta huduma ya maji.
Akizungumza wakati wa hafla ya utiaji saini mkataba na kumtambulisha Mkandarasi wa mradi huo, Mkuu wa Wilaya ya Same Kasilda Mgeni amemtaka Mkandarasi anayetekeleza mradi huo kuhakikisha utekelezaji wa mradi unafanyika kwa viwango vya utekelezaji wa miradi ya Serikali kwa kuzingatia mkataba unavyomtaka ili kusaidia kuondoa adha ya upatikanaji wa maji wanayokabiliana nayo kwa sasa wananchi wa Kata ya Kihurio.
Aidha Kasilda amesisitiza pia Wananchi wa Kihurio kuhakikisha wanatoa ushirikiano kwa Mkandarasi kwenye kipindi chote cha utekelezaji wa mradi, ikiwa ni pamoja na kila mmoja kuwa mlinzi wa kwanza wa mitambo itakayotumiwa na wakandarasi kutekeleza mradi huo.
“Namshukuru sana Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuendeleza jitihada zake za dhati za kumtua mama ndoo kichwani, mradi huu unaenda kuwa mkombozi kwa Wananchi wangu wa kihurio ambao kwa kipindi kirefu wamekuwa wakiteseka na kulazimika kutembea umbali mrefu kutafuta huduma ya maji kwenye mito”. Alisema Kasilda.
Pia amempongeze Mbunge wa Jimbo la Same Mashariki Anne Kilango kwa namna ambavyo anawapambania Wananchi wake kuhakikisha huduma mbalimbali za kijamii kwenye Jimbo lake zinaimalika.
Naye Mkurugenzi wa kampuni ya Fesam Construction Limited, Mhandisi Charles Maganga, ameahidi kuifanya kazi hiyo kwa wakati kulingana na mkataba unavyomtaka ili mradi uweze kutoa huduma kwa wananchi kama ilivyokusudiwa na Serikali.