Na. Ashura Mohamed -Arusha
Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi Profesa Riziki Shemdoe amewataka wafugaji nchini kubadili mfumo wa Ufugaji kwa Kufuga kisasa ili kupata mbari bora na mifugo yenye tija kwa maendeleo yao na taifa kwa Ujumla.
Shemdoe amesema kuwa Utumiaji wa teknolojia ya Uhimilishaji inaleta matokeo makubwa kwa wafugaji na kupelekea kupata mbari bora za mifugo bila ya mfugaji kupandisha kwa kutumia dume.
Katibu Mkuu Shemdoe ameyasema hayo Jijini Arusha wakati alipofanya Ziara ya Kutembelea wafugaji ambao ni wanufaika wa Miradi ya Enviro-Cow na AADGG ambayo ipo chini ya Wizara ya Mifugo na Uvuvi.
“Leo nimefarijika kutembelea wafugaji hawa ambao ni wanufaika wa miradi yetu miwili ya taasisi zetu za TALIRI na ILRI, ambapo mradi wa Enviro-cow una lengo la kufanya kazi ya utafiti wa kupunguza hewa ukaa na kuangalia ng’ombe wanavyolishwa na namna wavyochangia katika uzalishaji wa hewa Ukaa.
Aidha, Profesa Shemdoe alisema kuwa mradi wa AADGG una lengo la kuimarisha mbari za mifugo ambapo teknolojia hiyo ya uhimilishaji inaleta matokea makubwa na mazuri.
Katika hatua nyingine, Afisa Utafiti Dkt. Eliamon Lyatuu kutoka Shirika la Utafiti wa Mifugo duniani (ILRI) alisema kuwa mradi wa AADGG ulikuwa na lengo la kutengeneza kanzi data ili kanzi data hiyo itumike kutoa mrejesho kwa wafugaji matokeo ya Uhimilishaji na baadae takwimu hizo zitumike katika kuchagua ng’ombe bora, jambo ambalo limefanikiwa kwa kiasi kikubwa.
“Huku kote tunapopita tunaona maziwa yameongezeka kwa asilimia 40 baada ya kuboresha usimamizi wa Mifugo,wala hawajabadilisha mifugo hivyo upimaji wa ubora wa mifugo ni muhimu ili kumsaidia mfugaji kupata tija na kupunguza gharama za uendeshaji hilo ndio lengo letu na mnaona wamefanikiwa kwenye hili.”Alisema Lyatuu
Baadhi ya wafugaji wa N’gombe akiwemo Bw. Ayub Meshili na bibi Neng’ida Mosses ambao ni wafugaji wa kijiji cha Ng’iresi kilichopo katika kata ya Bang’ata wilayani arumeru walisema kuwa miradi hiyo imewasaidia kuongeza tija katika Uzalishaji haswa wa Maziwa ambapo kwa siku wanapata wastani wa lita 60 tofauti na awali walikuwa wanapata lita 20 tu.
Hata hivyo, walisema kuwa kupitia mradi wa AADGG wameweza kuboresha mifugo yao na kujiunga katika vikundi na kupata soko la uhakika la maziwa katika moja ya kiwanda kilichopo mkoani Arusha.
Katibu mkuu profesa Riziki Shemdoe akiwa na mmoja wa Wafugaji Bi.Neng’ida Mosses wakati wa kutembelea wafugaji wilayani Arumeru.
Â
Â