Shirika lisilo la Kiserikali la Relief to Development Society (REDESO) linaendesha mafunzo ya matumizi ya nishati safi na salama kwa makundi ya mama lishe, wakulima wa mbogamboga, na madereva wa bodaboda 250.
Lengo la mafunzo haya ni kubadili mtazamo kuhusu matumizi ya nishati chafu ili kuunga mkono jitihada za serikali kupambana na mabadiliko ya tabianchi.
Mafunzo haya yanafanyika katika Ukumbi wa Halmashauri ya Mji Kibaha, yakilenga kuhamasisha matumizi ya nishati safi kwa gharama nafuu na endelevu kwa kutumia rasilimali zinazopatikana katika mazingira husika.
Mkurugenzi Mtendaji wa REDESO, Abeid Kasaizi, alisema shirika limeanza katika kata ya Mkuza, Kibaha, ambapo asilimia 62 ya watu waliohojiwa kuhusu nishati safi walikiri kutoitambua.
Kasaizi aliongeza, lengo la kuchagua kundi la vijana wa bodaboda ni kuwawezesha kuhama kutoka kwenye matumizi ya mafuta kwenda kwenye gesi na umeme.
Aidha, kundi la mama lishe linahamasishwa kuacha kutumia kuni na mkaa na badala yake kutumia majiko banifu yanayotumia mkaa kidogo au teknolojia nyingine rafiki kwa mazingira.
Kasaizi alieleza REDESO, kwa ufadhili wa International Development Research Centre (IDRC/CRDI) kutoka Canada, itaendelea kutoa mafunzo hayo kwa Watanzania kupitia vyuo vya VETA, ikiwa ni sehemu ya kuunga mkono juhudi za Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, ambaye hivi karibuni ametangazwa kuwa kinara wa nishati safi na salama barani Afrika.
Mzumbe Mussa, mtaalam wa nishati safi na salama, ameeleza kuwa nishati safi ni ile inayozalishwa kutokana na vyanzo rafiki kwa mazingira, visivyochafua hewa, maji, na ardhi.
Alitaja aina za nishati hizi kuwa ni jua, upepo, maji, jotoardhi, na nishati inayotokana na viumbe hai.
Debetria Dionizi, mmoja wa washiriki wa mafunzo, amelipongeza shirika hilo kwa kutoa mafunzo haya, akisema kwamba yamekuja kwa wakati muafaka kwani matumizi ya nishati safi yatamuepusha na madhara ya kiafya, kupunguza gharama za kuni na mkaa, na kumwezesha kupata kipato .
Aliiomba serikali kuweka ruzuku katika ununuzi wa gesi.