Kamanda wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Mwanza Wilbroad Mutafungwa akizungumza na waandishi wa habari (hawapo pichani)
…….
Na Hellen Mtereko, Mwanza
Jeshi la Polisi Mkoani Mwanza linamtafuta mtu mmoja aliyejulikana kwa jina moja la Jackson maarufu (Mjomba) Mkazi wa Nansio Wilaya ya Ukerewe Mkoani hapa kwa tuhuma za mauaji ya Tatu Daniel (9) ambaye ni mwanafunzi wa darasa la pili Shule ya msingi Nabweko aliyeuawa kwa kukabwa shingoni kisha kubakwa.
Hayo yamebainishwa leo Ijumaa Novemba 08, 2024 na Kamanda wa Jeshi hilo Wilbroad Mutafungwa wakati akitoa taarifa ya tukio hilo kwa waandishi wa habari.
Alisema Novemba 04, 2024 katika kijiji cha Nabweko ulionekana mwili uliotambuliwa na wazazi wake ambao ni Hamis Mpandwe (39) na rehema Peter (43) wakazi wa Nabweko kisiwa cha Irugwa ambapo mwili huo ulikuwa umetelekezwa kwenye jengo ambalo halijakamilika kujengwa.
“Inadaiwa Novemba 3 mwaka huu majira ya saa mbili kamili Marehemu Tatu Daniel alikuwa anacheza na wenzake ndipo alitokea Jackson ambae ni rafiki wa baba wa marehemu akamchukua kwa ahadi ya kwenda kumnunulia pipi dukani ndipo akatoweka nae kusiko julikana hadi mwili wake ulipopatikana akiwa amefariki Dunia”, Alisema Kamanda Mutafungwa
Mwisho Kamanda Mutafungwa aliwataka wananchi kushirikiana na Jeshi la Polisi kwakutoa taarifa itakayofanikisha kukamatwa kwa mtuhumiwa huyo ili hatua kali za kisheria ziweze kuchukuliwa dhidi yake.