Na Linda Akyoo-Same
Mkuu wa Wilaya ya Same Mhe.Kasilda Mgeni amewaonya Wananchi kuacha mara moja tabia ya kueneza Imani potofu kwenye jamii zinazosababisha moto kutokea kwenye misitu.
Amesisitiza kuwa Serikali haitasita kuchukua hatua kali kwa yeyote atakaye bainika kuendeleza vitendo hivyo,kwani vinasababisha kuwepo kwa uharibifu mkubwa wa Mazingira na kufanya viumbe hai vipotee na kupoteza kabisa uoto wa Asili kwenye misitu ya Asili.
DC Kasilda ameyasema hayo leo tarehe 08 Novemba,2024 wakati akifunguwa mafunzo ya ufuatiliaji mioto katika hifadhi za misitu, yanayolenga kuboresha utayari wa Taasisi ya TFS katika kudhibiti matukio ya moto kwenye Hifadhi za Mazingira Asilia, Hifadhi za Misitu na Misitu ya kupandwa.
Aidha DC Kasilda amesema kuwa mafunzo haya yamekuja wakati muafaka sana,kwani amekuwa akitembea kwenye ziara zake mbalimbali ndani ya Wilaya ya Same kati ya jambo ambalo lilikuwa linamchefua sana ni namna ambavyo Wananchi wamekuwa wakichoma moto hovyo,jambo ambalo linasababisha kuharibu mazingira ikiwemo maeneo ya Hifadhi.
Sambamba na hilo DC Kasilda amesisitiza kuwa pamoja na Wilaya kuchukua hatua za makusudi za kukabiliana na watu wanaoharibu Mazingira kwa kuchoma moto,lakini pia jitihada za pamoja baina ya Serikali ya Wilaya na Taasisi za uhifadhi zinahitajika kuhakikisha wahusika wote wanachukuliwa hatua ili misitu iweze kubaki salama.
Hata hivyo DC Kasilda ameielekeza TFS kushirikiana na vyombo vya usalama, ikiwemo chombo chenye dhamana,Jeshi la Zimamoto na uokoaji kunapotokea matukio makubwa ya mioto ili waweze kusaidia kuongeza nguvu na kuokoa sehemu ya mazingira dhidi ya majanga hayo.
Kwa upande wake Kaimu kamanda wa Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) Kanda ya Kaskazini Agustine Mathias amesema miongoni mwa sababu za kutokea kwa matukio hayo ya moto ni imani potofu kwa baadhi ya watu ambao wanashindana kuchoma moto na yule ambaye moto wake utaenda mbali kwamba yeye anaonekana ataishi muda mrefu sana kuliko wenzake.
Sambamba na hilo shughuli za kijamii ikiwemo uandaaji wa mashamba, Uvunaji holela wa asali, Uchomaji wa Mkaa na Uwindaji wa Wanyama pori, nazo zinachangia.
Takribani Hekta 470 za Hifadhi kanda ya Kaskazini inayojumuisha Mikoa ya Tanga, Kilimanjaro, Arusha na Manyara zimeathiriwa na moto katika kipindi cha msimu huu wa kiangazi kati ya hizo takribani Hekta 132 zipo Wilaya ya Same Mkoani Kilimanjaro ikiwemo baadhi ya maeneo ya Hifadhi ya Msitu Asilia wa Chome (Shengena).