Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Ali Mwinyi, anatarajiwa kuzindua Jengo la Ofisi na Maabara za Tume ya Nguvu za Atomu Tanzania (TAEC) katika eneo la Dunga – Zuze, Zanzibar, Novemba 11, 2024, kuanzia saa 5 asubuhi.
Akizungumza na waandishi wa habari Novemba 7, 2024 jijini Dodoma, Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Adolf Mkenda, alisema kuwa uzinduzi huo ni sehemu ya mpango wa Wizara ya Elimu kwa kushirikiana na TAEC katika kusogeza huduma za teknolojia ya nyuklia kwa wananchi. Katika hatua hiyo, TAEC imeanzisha ofisi na maabara za nyuklia katika kanda nne: Kanda ya Kaskazini (Arusha), Kanda ya Kati (Dodoma), Kanda ya Ziwa (Mwanza), na sasa, Zanzibar.
Prof. Mkenda alifafanua kuwa lengo la kujenga ofisi hizo ni kuhakikisha huduma za TAEC zinapatikana karibu na wananchi katika kanda mbalimbali. “Nimewaita hapa ili niwaeleze wadau na umma wa Watanzania kuhusu uzinduzi wa Maabara na Ofisi za Tume ya Nguvu za Atomu Tanzania (TAEC) zilizojengwa Dunga Zuze, Zanzibar,” alisema Waziri Mkenda.
Hatua hiyo ni utekelezaji wa maelekezo ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, ambaye alihimiza kuimarishwa kwa huduma, tafiti na ubunifu unaolenga kuongeza matumizi ya sayansi na teknolojia ya nyuklia katika sekta mbalimbali nchini.
Prof. Mkenda alieleza kuwa teknolojia ya nyuklia inaweza kuchangia kwa kiasi kikubwa katika sekta nyingi kama ikitumika kwa usahihi. Alitoa mfano wa matumizi ya teknolojia hii katika kugundua na kutibu saratani, kuboresha mbegu za mazao, kuua vimelea vinavyosababisha chakula kuharibika, na kudhibiti uzalishwaji wa wadudu waharibifu kama mbung’o.
Aidha, alikumbusha kuwa kutokana na manufaa haya ya teknolojia ya nyuklia, Serikali imeanzisha mpango wa ufadhili kupitia ‘Samia Extended Scholarship’ kwa ajili ya vijana wa Kitanzania kusoma nje ya nchi katika ngazi ya umahiri kwenye masuala ya Sayansi na Teknolojia ya Nyuklia. Kuanzia mwaka huu, vijana watano watapata ufadhili kwa ajili ya shahada hizi.
Prof. Mkenda alihitimisha kwa kusema kuwa Serikali itaendelea kuongeza kiwango cha ufadhili kwa kushirikiana na wadau ili kuhakikisha nchi inakuwa na wataalamu wa kutosha katika nyanja husika.