Mkuu wa mkoa wa Katavi bi. Mwanamvua Mrindoko wakati akizungumza na vyombo vya habari.
………….
Na Zillipa Joseph, Katavi.
Mkuu wa mkoa wa Katavi bi. Mwanamvua Mrindoko amewashukuru wakazi wa mkoa huo kwa hali ya amani wakati ambapo Taifa linaelekea kufanya uchaguzi wa serikali za mitaa Novemba 27 mwaka huu.
Bi. Mrindoko ambaye pia ni mwenyekiti wa usalama mkoa huo amesema amepata ushirikiano mkubwa kutoka kwa wananchi tangu kipindi cha kujiandikisha katika daftari la makazi hadi sasa.
Amewashauri wadau wa uchaguzi, vyama vya siasa na wasimamizi wa uchaguzi waendelee kusimamia kanuni, sheria na taratibu za uchaguzi kama zilivyowekwa na Wizara ya Tawala za mikoa na serikali za mitaa (TAMISEMI).
Aliongeza kuwa kwa wale ambao watakuwa na mapingamizi wafuate kanuni za kukata Rufaa.
Aidha Mkuu huyo wa mkoa wa Katavi amewataka wasimamizi wa uchaguzi kihakikisha wanatoa haki kwa wadau wote wa uchaguzi.
Ametoa onyo kwa yeyote mwenye nia ovu ya kutaka kuhatarisha usalama kuwa atashughulikiwa na vyombo vya dola.
Alisisitiza kuwa mkoa umejipanga vyema kuhakikisha usalama wa raia na mali zao unaendelea kuwepo wakati wa uchaguzi na hata baada ya uchaguzi.