-AWAKUMBUSHA WANUFAIKA WA MIKOPO YA MFUKO WA WANAWAKE KUFANYA MAREJESHO.
-AWAASA WANAWAKE KUJITOKEZA KUGOMBEA NAFASI ZA UONGOZI
Na WMJJWM, Dodoma
Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake, na Makundi Maalum, Felister Mdemu amepongeza juhudi za wanawake katika kujikwamua kiuchumi kwa kuanzisha miradi mbalimbali baada ya kupatiwa mikopo kutoka Serikalini kupitia Mfuko wa Maendeleo ya Wanawake (WDF).
Mdemu ametoa wito huo katika ziara ya kutembelea miradi ya wanawake walionufaika na mikopo ya Mfuko wa Maendeleo ya Wanawake, inayosimamiwa na Wizara, Novemba 08, 2024 jijini Dodoma.
“Nichukue nafasi hii kuwapongeza wale wote mlionufaika na mikopo na mmeweza kuanzisha na kusimamia miradi yenu ambayo imekuwa chachu ya kujikwamua kiuchumi. Hongereni sana! Hii ndiyo dhamira ya Rais wetu, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kupitia Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake, na Makundi Maalum kuwainua wanawake kiuchumi. Ndiyo maana leo tupo hapa kuwatembelea na kujionea maendeleo yenu.” amesema Mdemu
Pia Mdemu amewasisitiza kuhakikisha wanafanya marejesho ya mikopo hiyo ili kutoa fursa kwa wanawake wengine kunufaika, aidha amewataka wajitokeze katika kugombea nafasi mbalimbali kupitia uchaguzi wa Serikali za mitaa na uchaguzi mkuu mwaka ujao 2025.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Msaidizi wa Idara ya Maendeleo ya Jinsia, Juliana Kibonde amesema kuwa Wizara itaendelea kuwatembelea wanufaika wote wa mikopo hiyo ili kufuatilia maendeleo yao, kujua changamoto wanazokutana nazo na kutafuta njia bora za kuzitatua.
Amongeza kuwa Wizara inaendelea kutoa mikopo kwa wanawake kupitia Mfuko wa Maendeleo ya Wanawake (WDF) ili kuwasaidia kuanzisha na kukuza miradi ya kiuchumi.
Baadhi ya wanufaika wa mikopo hiyo wameishukuru Serikali chini ya uongozi wa Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuwawezesha kupitia mikopo yenye masharti nafuu na rafiki, ambayo imewasaidia kuanzisha miradi inayoleta kipato na kuimarisha maisha ya familia zao.
Aidha, wameahidi kuendelea kufanya marejesho kwa mujibu wa taratibu ili wanawake wengine wapate nafasi ya kunufaika na mikopo hiyo.