Na Karama Kenyunko Michuzi Tv
JUMLA ya watahiniwa 557,731 wanatarajiwa kuanza kufanya mtihani wa Taifa wa kidato cha nne kuanzia kesho Jumatatu Novemba 11 hadi Novemba 15, 2024 ambapo kati yao 529,321 ni wa shule na watahiniwa wa kujitegemea ni 28,410
Mtihani huo utafanyika katika shule za sekondari 5585 na vituo vya watahiniwa wa kujitegemea 961 .
Katibu Mtendaji wa Baraza la Mitihani la Tanzania (NECTA), Dkt. Said Mohamed amesema hayo leo Novemba 10, jijini Dar es Salaam alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari kuhusu maandalizi ya mtihani huo.
Dkt Mohamed amesema katika watahaniwa wa shule 557,731 waliosajiliwa kufanya mtihani huo wavulana ni 250,562 sawa na asilimia 47.34 na wasichana ni 278,759 sawa na asilimia 52.66.
“Aidha watainiwa wa shule wenye mahitaji maalum 1,088 waliosajiliwa kati yao 601 ni wenye uoni hafifu, 56 ni wasioona, 209 wenye ulemavu wa kusikia, 39 ni wenye ulemavu wa akili na 183 ni wenye ulemavu wa viungo vya mwili,”amesema Mohamed
Amesema, Watahiniwa wa kujitegemea 28,410 wamesajiliwa ambapo kati yao wavulana ni 11,167 sawa na asilimia 39.31 na wasichana 17,243 sawa na asilimia 60.69 huku kwa wenye mahitaji maalum wakiwa 18 kati yao mwenye uoni hafifu ni mmoja, wasioona 16 na mwenye ulemavu wa viungo mmoja.
Dkt Mohamed amesema maandalizi yote kwa ajili ya mtihani yamekamilika ikiwa ni pamoja na kusambazwa kwa mtihani ,vijitabu vya kujibia na nyaraka zote muhimu zinazohusu mitihani husika katika mikoa yote Tanzania Bara na Zanzibar.
Aidha Dkt. Mohamed ametoa wito kwa kamati za mitihani za mikoa na Halmashauri kuhakikisha usalama wa vituo vya mitihani unaimarishwa na vinatumika kwa mujibu wa mwongozo uliotolewa na Baraza.
“Kwa upande wa wasimamizi walioteuliwa kusimamia mtihani wahakikishe wanafanya kazi yao ya usimamizi kwa umakini na uadilifu wa hali ya juu. ”Amesema Dkt. Mohamed
Kwa upande wa watahiniwa, Baraza hilo limewataka kufanya mitihani kwa kuzingatia kanuni za mitihani na kueleza kuwa halitarajii kuona mtahiniwa yoyote kujihusisha na vitendo vya udanganyifu.
“Mtahiniwa yoyote atakayebainika kufanya udanganyifu, matokeo yake yatafutwa kwa mujibu wa kanuni za mtihani,”amesisitiza .
Kwa upande wa wamiliki wa shule na wakuu wa shule, Dkt. Mohamed amesema kuwa wanapaswa kutambua kuwa shule zao ni vituo maalumu vya mitihani hivyo kwa namna yoyote hawatakiwi kuingilia majukumu ya wasimamizi wa mtihani katika kipindi chote cha ufanyikaji wa mtihani huo.
Amesema baraza halitosita kikifuta kituo chochote cha mtihani endapo litajiridhisha pasipo shaka kuwepo wa matukio au vitendo vinavyohatarisha usalama wa mtihani.
“Aidha wakuu wa shule wahakikishe wanatekeleza majukumu yao ya usimamizi kwa kuzingatia mwongozo wa usimamizi uliotolewa na Baraza na kuepeuka kuingilia usimamizi wa watahiniwa ndani ya vyumba vya mitihanii.” Amesema.
Pia baraza hilo limetoa wito kwa jamii kutoa ushirikiano unaotakiwa kuhakikisha mtihani wa kidato cha nne na maarifa 2024 unafanyika kwa amani na utulivu.
“Wananchi wanaombwa kuhakkikisha kuwa hakuna mtu yoyote asiyehusika na mtihani anaingia kwenye maeneo ya shule katika kipindi chote cha mtihani kwani kwa kufanya hivyo tuatawezesha wanafunzi kufanya mtihanni kwa amani na utulivu”. Amesema amesema