Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Mahmoud Thabit Kombo (Mb.) amesisitiza kuwa Wizara yake itaendeleza jitihada za kutafuta fursa za Lugha ya Kiswahili duniani kupitia Balozi zake nje.
Msisitizo huo umetolewa wakati akitoa salamu kwenye hafla ya ufunguzi wa Kongamano la Kimataifa la Kiswahili linalofanyika jijini Havana, Cuba na kuhudhuriwa na washiriki wapatao 400 kutoka sehemu mbalimbali duniani pamoja na wadau wa Kiswahili kutoka Tanzania.
Kongamano hili ni matokeo ya jitihada zinazofanywa na Balozi za Tanzania ikiwemo Ubalozi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania nchini Cuba uliofanikisha kufanyika kwa tukio hili muhimu ambalo ni utekelezaji wa jukumu la Wizara la kubidhaisha Kiswahili duniani. Jitihada hizo zinaenda sambamba na zile zilizowezesha kutambulika kwa Kiswahili na kupewa tarehe maalum ya kuadhimishwa duniani ambayo ni tarehe 7 Julai ya kila mwaka.
‘’Kiswahili kinahitaji ushindani ili kiendelee kukua hivyo nitoe rai kwenu wataalamu na wadau wa Kiswahili kujifunza lugha nyingine ili kurahisisha zoezi la kufundisha na kusambaza Kiswahili kwa wageni. Pia Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki itaendele kutoa fursa za Kiswahili duniani kupitia Balozi zake, hivyo, ni jukumu la pamoja kuhakikisha fursa hizo zinatumika kikamilifu”, alisisitiza Waziri Kombo.
Vilevile, Waziri Kombo ameeleza kuwa katika kuendeleza jitihada za kukuza Kiswahili, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan amekuwa akihutubia kwa lugha ya Kiswahili katika mikutano ya Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) na Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC). Wizara inaendelea na jitihada za kushawishi Kiswahili kitumike katika Jumuiya za Kikanda zingine ambazo Tanzania ni Mwanachama.
Waziri Kombo ametumia nafasi ya Kongamano hilo kumshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, pamoja na Rais wa Jamhuri ya Cuba, Mhe. Miguel Díaz-Canel kwa kuimarisha na kukuza ushirikiano ulioasisiwa na waasisi wa mataifa hayo mawili.
Pamoja na masuala mengine Waziri Kombo alitoa salamu za pole kwa Serikali ya Cuba kufuatia kutokea kwa Kimbunga Rafael ambacho kimeleta athari kadhaa nchini humo. Aidha, ameishukuru nchi ya Cuba kwa ukarimu uliotolewa na nchi hiyo licha ya changamoto inazopitia.
Kufuatia kuahirishwa kwa ziara ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia SuluhuHassan nchini Cuba, ufunguzi wa Kongamano hilo ulifanywa na Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mhe. Dkt. Damas Ndumbaro ambaye aliwasilisha hotuba ya ufunguzi kwa niaba ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Hotuba ya Mhe. Rais imesisitiza umuhimu wa lugha kama nyenzo muhimu katika kurahisisha mawasiliano na kurahisisha shughuli za kiuchumi ikiwemo biashara. Katika Hotuba yake hiyo, Rais Samia ametambua mchango wa Cuba katika harakati za ukombozi wa Bara la Afrika na kusema kufuatia umoja na mshikamano uliopo Tanzania itaendeleza ushirikiano wake na Cuba ikiwa ni pamoja na kulaani vikwazo vya kiuchumi vilivyowekwa na Marekani dhidi ya Cuba.
Naye Waziri wa Elimu ya Juu wa Cuba, Mhe. Walter Baluja Garcia aliishukuru Tanzania kwa kuiheshimisha Cuba kwa kuipa wenyeji wa Kongamano hilo, pia akaeleza katika kuendelea kukuza ushirikiano na mawasiliano kwa sasa Chuo Kikuu cha Havana kina wanafunzi 50 wa lugha ya Kiswahili.