Madiwani katika Baraza la Halmashauri ya Wilaya ya Geita limekutana kujadili mapendekezo ya mpango wa wajibu kwa kampuni ya Mgodi wa Dhahabu Geita (GGML) kwa jamii (CSR) 2024 katika utekelezaji wa Miradi ya Maendeleo ambapo kiasi cha shilingi Bilioni 4.3 kimependekezwa kupitishwa.
Katika Kikao hicho kimewakutanisha wawakilishi kutoka Kampuni ya Mgodi wa Dhahabu (GGML), Ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Geita, Katibu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Geita na Wataalam wa Halmashauri kimefanyika katika ukumbi wa Mikutano wa Halmashauri .
Kwa Mujibu wa Taarifa Halmashauri ya Wilaya ya Geita kwa kipindi cha miaka mitano imekuwa ikiingia makubaliano ya utekelezaji wa miradi na Mgodi wa Dhahabu wa Geita (GGML) kupitia mpango wa wajibu wa mmliki wa Leseni ya madini kwa jamii (CSR) ambapo kila mwaka Mkataba (MoU) ni Shilingi Bilioni 4,300,000,000 umekuwa ukisainiwa.
Utekelezaji wa wajibu wa kampuni kwa jamii (CSR) ni kwa mujibu wa kanuni kifungu Na 4-(1) cha mwongozo wa wajibu wa mmliki wa leseni wa mwaka 2023 ambapo kinamtaka mmliki wa leseni za madini kuandaa mpango madhubuti wa wajibu wake kwa jamii ambayo anaendesha Shughuli zake za uchimbaji wa Madini.
Aidha Madiwani katika Baraza hilo wamehoji uongozi wa Mgodi wa dhahabu kutokukamilisha miradi ya maendeleo katika mpango wa CSR wa mwaka 2021 hadi 2023 na kuagiza mpango huo utekelezwe ili wananchi waweze kunufaika na miradi ambayo haijaanza kutumika kutokana na mpango huo kutokukamilika kwa wakati.
Ukamilishaji wa miradi ya mipango wa nyuma umechukua muda mrefu kutokana na sababu mbalimbali badhi zikiwa ni mchakato wa manunuzi unaofanywa na mgodi kuchukua muda mrefu, fedha za utekelezaji wa miradi hiyo kutokuwa halisi na gharama stahiki za miradi ikiwa ni pamoja na wazabuni waliopewa kazi na GGML kushindwa kupeleka vifaa kwa gharama zilizoanishwa.
Katika baraza hilo, Mbunge wa Jimbo la Geita Mhe Dkt Joseph Kasheku Msukuma ameutaka uongozi wa Mgodi wa Dhahabu GGML kufuata taratibu kulingana na Mou wanazosaini ili kukamilisha miradi ya maendeleo
” Msiwe sababu ya kukwamisha miradi ya maendeleo kwa kutoa taarifa ambazo sio sahihi kwa viongozi wenu , ” Amesema Mhe Msukuma.
Kwa upande wake Mbunge wa Jimbo la Busanda Mhe Mhandisi Tumaini Magesa ameutaka uongozi wa GGML kuvitambua vijiji ambavyo mgodi unaingia ili viweze kuingia kwenye mchakato vianze kupata stahiki zake kama vilivyo vijiji vingine ambavyo mgodi umefika.
Naye Katibu wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Wilayani Geita Komredi Michael Msuya amewataka watumishi wa Mgodi wa Dhahabu wa Geita (GGML) wanaosimamia miradi ya CSR kuwa wazalendo.
“ Muwe wazalendo kwenye hii nchi ili kuwasaidia wananchi wa Geita waweze kunufaika , ” Cde Msuya.
Msuya amewaomba Wabunge waliohudhuria kikao hicho ambao ni Mhe Mhandisi Tumaini Magesa na Mhe Dkt Joseph Msukuma kuisaidia Halmashauri ili mifumo ya GGML ibadilike iwe na tija ili miradi viporo iweze kukamilika.
Akihitimisha kikao cha baraza hilo Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Geita Mhe Charles Kazungu amewataka wataalam na waheshimiwa madiwani kila mmoja kutimiza wajibu katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo.
Vilevile Mhe Kazungu amewataka watumishi wa Mgodi wa Dhahabu GGML wanaosimamia miradi ya Maendeleo ndani ya Halmashauri kushughulikia swala la vijiji ambavyo vinapaswa kunufaika na CSR kwa kushirikiana na Ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Geita ili viweze kuingia kwenye mpango wa CSR.
The post Baraza la madiwani Geita lalidhia kupitisha bilioni 4.3 mapendekezo ya CSR 2024. first appeared on Millard Ayo.