NA EMMANUEL MBATILO, MICHUZI TV
MAMLAKA
ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA) imefanya operesheni
katika maeneo mbalimbali nchini kati ya Oktoba na Novemba 2024, na
kufanikiwa kukamata kilogramu 1,066.105 za dawa za kulevya.
Akizungumza
na waandishi wa habari leo Novemba 12, 2024 Jijini Dar es Salaam,
Kamishna Jenerali wa Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za
Kulevya Tanzania (DCEA), Aretas Lyimo amesema mpaka sasa watuhumiwa 58
wamekamatwa kwenye operesheni hiyo.
“Katika
dawa za kulevya tulizozikamata ni pamoja na mililita 447 za dawa tiba
zenye asili ya kulevya, na tumeweza kuteketeza jumla ya ekari 157.4 za
mashamba ya bangi na lita 19,804 za kemikali bashirifu”. Amesema
Kamishna Lyimo
Aidha
amesema kuwa kati ya dawa hizo, kilogramu 687.32 za skanka na kilogramu
moja (01) ya hashishi zilikamatwa eneo la Goba, Dar es Salaam, zikiwa
zimefichwa ndani ya nyumba ya mtuhumiwa.
Amesema
uchunguzi umebaini kuwa wateja wengi wa skanka ni wanawake, ambao hudai
kutumia dawa hizo kupunguza msongo wa mawazo na kujistarehesha.
“Skanka
ni aina ya bangi yenye kiwango kikubwa cha sumu, inavyosababisha
madhara makubwa kiafya. Vilevile, hashishi ambayo hutengenezwa kwa
mchanganyiko wa maua na mafuta ya mbegu za bangi, inapovutwa huzalisha
kemikali hatari zinazoweza kusababisha magonjwa ya akili kwa haraka.
Mara nyingi jamii huamini kuwa watu wanaopatwa na magonjwa haya
wamerogwa”. Amesema
Pamoja
na hayo amesema katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Mwalimu Julius
Nyerere, Mamlaka ilikamata mililita 120 za dawa tiba zenye asili ya
kulevya aina ya Codein, zikiwa zinasafirishwa kwenda nje ya nchi, pamoja
na mililita 327 zilizokutwa nyumbani kwa mtuhumiwa eneo la Tabata
Kinyerezi.
“Dawa
hizi ziliingizwa nchini kinyume na taratibu, zikiwa zimewekwa chapa
bandia ya dawa za kuogeshea mbwa na paka ili kuepuka kubainika.
Kukamatwa kwa dawa hizi ni ishara ya uwepo wa tatizo la matumizi holela
ya dawa za tiba zenye asili ya kulevya, Hali hii inachangiwa na
kuimarika kwa udhibiti wa dawa za kulevya na kusababisha wafanyabiashara
na watumiaji kutumia dawa tiba ya kulevya kama mbadala wa dawa za
kulevya”. Kamishna Lyimo ameeleza.
Kamishna
Lyimo amesema mkoani Dodoma, Mamlaka imewakamata watuhumiwa wawili
Suleiman Mbaruku Suleiman (maarufu Nyanda), mwenye umri wa miaka 52, na
Kimwaga Msobi Lazaro (miaka 37) wakazi wa mtaa wa Kinyali, kata ya
Viwandani.
“Watuhumiwa
hao walikamatwa na jumla ya gramu 393 za heroin. Nyanda anafahamika
kama kinara wa biashara ya dawa za kulevya mkoani humo na amekuwa
akifuatiliwa kwa muda mrefu”. Amesema
Kupitia
operesheni za kanda, DCEA pia imekamata kilo 303.553 za bangi, gramu
103.8 za heroin, na kilo 63 za mirungi katika maeneo mbalimbali nchini.
Mamlaka
ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya inawaomba wananchi
waendelee kuunga mkono jitihada hizi kwa kufichua wafanyabiashara wa
dawa za kulevya na kuhamasishana kutoshiriki katika biashara na matumizi
ya dawa za kulevya.