Na Mwandishi Wetu, Mara
Mahakama ya Hakimu Mkazi Musoma, mkoani Mara, mbele ya Hakimu Mkazi Mfawidhi Veronica Mgendi, imefungua Kesi ya Uhujumu Uchumi Na. 32001/2024, ikiwahusisha Ofisa Utumishi wa Wilaya Nico Amanyisye Kayange na wenzake 11.
Washtakiwa hao wanakabiliwa na mashtaka ya kuendesha genge la uhalifu kinyume na Aya ya 4(1)(a) ya Jedwali la Kwanza na vifungu vya 57(1) na 60(2) vya Sheria ya Uhujumu Uchumi na Makosa ya Kupangwa, Sura ya 200, Mapitio ya mwaka 2019. Aidha, wanatuhumiwa kwa matumizi mabaya ya mamlaka kinyume na kifungu cha 31 cha Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa, Sura ya 329, pamoja na kusababisha hasara ya Shilingi 205,720,071 kinyume na Aya ya 10(1) ya Jedwali la Kwanza na vifungu vya 57(1) na 60(2) vya Sheria ya Uhujumu Uchumi, marejeo ya mwaka 2019.
Kati ya watuhumiwa 12, tisa ni watumishi wa Halmashauri ya Wilaya ya Bunda, wakiwemo Amos Jeremiah Kusaja (aliyekuwa Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya), Nico Amanyisye Kayange (Ofisa Utumishi wa Wilaya), Mona Shomary Bitakwate (Ofisa Utumishi), Sangi Makenge Ruge (Mwekahazina wa Wilaya), Emmanuel Simon Mboje (Mkuu wa Idara ya Manunuzi), Abbas Ndyamukama na Shaban Shissebe Ndalu (Mhasibu), Hesbone Pius Bature (Mhasibu Msaidizi), na Nuru Yahya Yunge (Mganga Mkuu wa Wilaya).
Watuhumiwa wengine watatu ni wazabuni, ambao ni Thomas Michael Kweka, Gabriel Mugini Kenene, na Mseti Masanchu Maswi.
Mwendesha Mashtaka wa TAKUKURU, Restituta Kessy, akishirikiana na Zena Kisesa, walisoma hati ya mashtaka mnamo Novemba 11, 2024. Walidai kuwa washtakiwa hao, kwa tarehe tofauti kati ya Juni na Julai 2021, walitumia vibaya mamlaka yao kwa kutofuata taratibu za manunuzi na kufanya malipo kwa wazabuni bila vifaa vya ujenzi kusambazwa katika mradi wa jengo la utawala la Halmashauri ya Wilaya ya Bunda, na hivyo kuisababishia hasara halmashauri hiyo ya Shilingi 205,720,071.
Washtakiwa wote wamekana mashtaka yanayowakabili, na kesi hiyo imeahirishwa hadi Desemba 2, 2024, kwa ajili ya kusomwa hoja za awali. Washtakiwa wamepata dhamana na kuachiwa kwa masharti ya dhamana.