Na Ashrack Miraji, Fullshangwe Media
Mkuu wa Wilaya ya Tanga, Mhe. Kubecha, amesema pambano la ngumi litakalofanyika jijini Tanga tarehe 16 mwezi huu linatarajiwa kuwa tukio la kihistoria ambalo litachangia pakubwa kukuza mchezo wa ngumi na vipaji vya mabondia, siyo tu kwa mkoa wa Tanga bali pia kwa nchi nzima.
Akizungumza na waandishi wa habari, Kubecha alieleza kuwa Mafia Boxing Promotion wamekuwa wadau muhimu katika kukuza mchezo wa ngumi, hasa katika mkoa wa Tanga na Tanzania kwa ujumla. Alisema kuwa, baada ya kukubaliana na wadau hao, waliamua kuandaa pambano hili kubwa Tanga ili kuwapa mabondia wa ndani na nje nafasi ya kushindana na kuvutia wapenzi wa ngumi.
“Tanga ni moja ya mikoa yenye hamasa kubwa kwa mchezo wa ngumi. Hivyo, niliamua kushirikiana na Mafia Boxing Promotion ili kuandaa pambano hili. Tunatarajia kuwakaribisha mabondia wa kimataifa na wa hapa nyumbani kwa pambano hili,” alisema Kubecha.
Mhe. Kubecha aliongeza kuwa pambano hili litakuwa kivutio kikubwa kwa wapenzi wa mchezo wa ngumi na fursa ya kuhamasisha wananchi kujitokeza kwenye uchaguzi wa Serikali za Mitaa, kwa kauli mbiu: “Ngumi yangu, Uchaguzi wangu, Maendeleo yangu.”
“Kwa niaba ya serikali, tunatoa wito kwa wakazi wa Tanga na mikoa jirani kujitokeza kwa wingi kuunga mkono mabondia wetu. Pambano hili linatarajiwa kuwa la kihistoria na litatoa ajira kwa vijana wa hapa,” alisema Kubecha.
Alithibitisha kuwa serikali imejipanga kikamilifu kuhakikisha usalama wa wananchi na wapenzi wa ngumi. “Tunahakikisha kila mmoja anahudhuria kwa amani na furaha, na kwamba ulinzi utakuwa wa kutosha kwa familia zote zinazokuja,” aliongeza.
Mhe. Kubecha alihitimisha kwa kueleza kuwa mchezo wa ngumi ni zaidi ya ushindani, kwani unajenga urafiki, mshikamano, na kuwahamasisha vijana kujituma kwa ajili ya taifa lao. Aidha, alisema mchezo wa ngumi unatoa fursa kwa vijana kuwakilisha nchi kimataifa, hivyo kuitangaza Tanzania kwenye anga za michezo.