Na Khadija Kalili Michuzi Tv
TAASISI ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Mkoa wa Pwani imefanikisha kukusanya kiasi cha shilingi bilioni 1.5 ambayo ni michango ya wafanyakazi kupitia Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF) kutoka kwa waajiri walioshindwa kuingiza michango ya wafanyakazi.
Hayo yalisemwa leo na Naibu Mkuu wa TAKUKURU Alli Sadiki alipozungumza na waandishi wa habari ofisini kwake Mjini Kibaha wakati akitoa taarifa ya kipindi cha Julai hadi Septemba 2024.
Sadiki amesema kuwa TAKUKURU iliingilia kati katika mfumo wa ukusanyaji wa michango ya waajiri ambao walikuwa hawapeleki michango ya waajiriwa kupitia NSSF.
“Meneja wa NSSF Pwani alilalamikia upotevu wa makusanyo kama michango ya waajiri inayosababisha upotevu wa fedha na usumbufu kwa wastaafu kutolipwa mafao yao kwa wakati,”amesema Sadiki.
Aidha amesema kuwa uzuiaji huo umefanyika baada ya kuwatafuta waajiri 77 ambao walikuwa na deni la michango ya Shilingi bilioni 7.5 ambapo Takukuru imeingilia kati kuhusu ukusanyaji wa michango ndipo wadaiwa na NSSF walikubaliana ifikapo Julai 24 mwaka huu walipe deni hilo kwa asilimia 20.
“Wakati huohuo TAKUKURU wamefanya uchambuzi wa mfumo mmoja katika eneo la upatikanaji wa huduma na dawa kwa wagonjwa wanaotumia bima ya NHIF kwenye hospitali, vituo vya afya na zahanati za serikali na binafsi katika Halmashauri ya Mji Kibaha. Katika chambuzi huu wa mfumo uliofanyika mapungufu yaliyobainika na tayari hatua zimechukuliwa” amesema Sadiki.
Ameongeza kwa kusema kuwa katika eneo la uzuiaji rushwa wamefanya kazi ya ufuatiliaji miradi 53 ya maendeleo yenye thamani ya Bil.14,490,667,779.32 katika sekta za afya, elimu, maji na barabara.
Sadiki amesema kuwa TAKUKURU Mkoa wa Pwani wamejipanga kuendelea kutoa elimu madhara ya rushwa katika uchaguzi kupitia semina,mikutano ya hadhara na vipindi vya redio ili kuwafikia wadau wote wanaoshiriki kwenye uchaguzi. Lengo ni kushiriki uchaguzi usiokuwa na vitendo vya rushwa,pia tutaendele kufanya udhibiti wa mapato ya serikali na usimamizi wa rasilimali za umma ikowq ni pamoja na ufuatiliaji wa fedha zinazotolewa na serikali kwa ajili ya kutekeleza miradi ya maendeleo tutaendelea kupokea taarifa za vitendo vya rushwa kufanya uchunguzi na kufukisha watuhumiwa Mahakamani.
TAKUKURU Mkoa wa Pwani imetoa wito kwa wananchi kuendelea kuunga mkono jitihada za mapambano dhidi ya rushwa kwa kufichua wale wote wanaoshiriki kufanya vitendo vya rushwa kwa kutoa taarufa sahihi zitakazowezesha kuwachukulia hatua wahusika hasa katika kipindi hiki cha kuelekea uchaguzi wa Serikali za Mitaa mwaka huu.
“Nawaasa wananchi kufuata sheria kanuni na taratibu zilizowekwa ili kuwa salama na kuepuka migogoro yenye kuleta viashiria vya rushwa”amesema Sadiki.
Amesema kuwa katika kipindi cha Julai na Septemba TAKUKURU wamepokea malalamiko 88 kati ya hayo malalamiko 68 yalihusu rushwa na taarifa hizo zimeshughulikiwa kwa mujibu wa sheria kwa kuanzisha uchunguzi ambao upo katika hatua mbalimbali za uchunguzi.
“Taarifa 20 zilizobaki ambazo hazikuhusu rushwa zimeshughulikiwa kwa njia ya uelimishaji,uzuiaji, ushauri na kuhamishiwa idara ingine. Taarifa hizo zimepokelewa kwa mchanganuo ufuatao TAMISEMI 20 Mifugo/Uvuvi 4,Elimu 21,Polisi 5,Ardhi 6,Fedha 2,Maji1,Mahakama 4 ,binafsi 2,Misitu2,AMCOS1,Usafirishaji 2 Viwanda 1,Vyama vya wafanyakazi 1,Ujenzi 2,Afya7,Siasa 1,Manunuzi 1 na Maendeleo ya Jamii 2 pia tumefungua kesi mpya 22 Mahakamani huku kesi 12 washtakiwa wametiwa hatiani.