Meneja wa TMDA Kanda ya Ziwa Mashariki, Sophia Mziray akizungumza wakati wa kukabidhi Maabara Hamishika kwa ajili ya kufanya Uchuguzi wa awali wa ufanisi wa Dawa katika hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Simiyu.
Muonekano wa Maabara Hamishika (Min Lab Kit) iliyokabidhiwa katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Simiyu
Baadhi ya Wafanyakazi na wageni kutoka Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Simiyu.
Mkuu wa Mkoa wa Simiyu Bw. Kenan Kihongosi akikata utepe katika tukio la ufunguzi wa Maabara Hamishika (Min Lab Kit) ya uchunguzi wa sampuli za dawa za magonjwa ya kipaumbele katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Simiyu. (Kulia) ni Meneja wa TMDA Kanda ya Kanda ya Ziwa Mashariki, Bi.Sophia Mziray.
…………………
NA MWANDISHI WETU, SIMIYU.
MAMLAKA ya Dawa na Vifaa Tiba (TMDA) imefungua kituo cha kufanya uchunguzi wa awali wa sampuli za dawa za kutibu magonjwa ya kipaumbele ikiwemo malaria, kifua kikuu na makali ya virusi vya ukimwi kwa kutumia Maabara Hamishika ( MIN LAB KIT) katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Simiyu tarehe 11 Novemba, 2024.
Katika tukio hilo Meneja wa TMDA Kanda ya Ziwa Mashariki, Bi. Sophia Mziray ameweza kumkabidhi Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Bw. Kenan Kihongosi maabara hamishika hiyo yenye thamani ya takribani shilingi Milioni 40.
Awali Meneja huyo wa Kanda amebainisha kuwa, Faida za kuwa na Maabara hiyo itarahisisha uchunguzi wa sampuli za dawa kutoka katika soko kwa eneo hilo na hivyo kuendelea kuwahakikishia wananchi ubora, usalama na ufanisi wa dawa nchini na hivyo kulinda afya ya jamii.
Aidha, Katika tukio hilo pia limeshuhudiwa na watendaji mbalimbali wakiwemo Katibu Tawala Bi. Prisca Kayombo, Mganga Mkuu wa Mkoa Dkt. Boniface na Mganga Mfawidhi hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Simiyu Dkt. Ndabakubi.