Na Sophia Kingimali.
SHIRIKA lisilo la kiserikali la Plan International kupitia mradi wake wa Play Matters limefanikiwa kufikia shule 31 zilizopo katika Halmashauri ya kibondo mkoa wa Kigoma na kutoa elimu kwa walimu jinsi ya kufundisha watoto kwa kutumia michezo ili kujenga uelewa kwa watoto hao na kuwafanya wapende shule.
Akizungumza na Mwandishi wa habari hii Novemba 13,2023 jijini Dar es salaam Afisa ufuatiliaji,tathimini,uwajibikaji na kujifunza wa Mradi wa Play Matters Mustapha Isabuda amesema mradi huo ni mahususi kwa ajili ya shule zilizopo ndani ya kambi ya wakimbizi lakini na zile zinazozunguka kambi hizo.
“Mradi huu kwa asilimia 60 ni shule zilizopo ndani ya kambi ya wakimbizi kwani ndio walengwa haswa lakini asilimia 40 ni shule za serikali zinazozunguka kambi za wakimbizi”,Amesema.
Aidha ameongeza kuwa walimu wanafundishwa mbinu hizo kwa kushirikiana na taasisi ya elimu Tanzania ambapo baada ya mafunzo wanaendelea na shughuli zao za ufudhishaji ambapo wadhibiti ubora wa shule katika Halmashauri wanatumika kufuatilia walimu pindi wanapofundisha kwa kutumia mbinu hizo.
“Tunasisitiza kutumia mbinu za michezo katika kuwafundisha watoto kwani inasaidia watoto kuelewa kwa haraka kwani wanakuwa wanashiriki moja kwa moja katika michezo lakini hata anaporudi nyumbani tunawasihi wazazi wawasaidie pindi wanapoona wanafanya vitu ambavyo wametumwa shule mfano vizibo n.k”,Amesema Isabuda.
Ameongeza kuwa katika kuhakikisha wanaendelea kumsaidia mtoto kwa njia ya michezo wanawashirikisha viongozi wa kijamii ili waweze kuwa mabarozi wazuri wa kueneza mbinu hizo pindi wanapokuwa na vikao vyao lakini pia wanawashirikisha na mabarozi wa michezo waliondani ya kambi na nje ya kambi hizo ili kwa kutumia michezo waeneze mbinu hizo.
Amesema kuna baadhi ya maeneo watoto hawapendi shule kwa sababu tu hakuna kinachomvutia kwenda kusoma lakini kwa kutumia mbinu ya michezo(Play Matters) inawavutia watoto wengi kupenda shule.
Akizungumzia kuhusu mradi huo wa Play Matters amesema lengo kubwa ni kuwajengea uwezo walimu wa awali na msingi kutumia mbinu ya michezo wakati wa ufundishaji wa wanafunzi darasani.
Amesema pia,mradi huo unatoa usaidizi katika shule kwani mpaka sasa wamesaidia shule 14 zilizopo katika manispaa ya kibondo ambapo wamezipatia compyuta mpakato pamoja na ptojecta lengo likiwa kuunga mkono serikali katika kuhamasisha matumizi ya teknolojia.
“Mradi wa Play Matters haujengi unasaidia changamoto ndogo ndogo ambazo zinaweza kuwa kikwazo kwa mwalimu kufundisha kwani kuna baadhi ya shule tuliweka simenti kwenye darasa na mambo mengine lakini lengo letu kuondoa vikwazo kwa walimu kushindwa kufundisha kwa kutumia mbinu ya michezo”,Amesema.
Aidha ameongeza kuwa mradi huo unafadhiliwa na The Legal Foundation unatekelezwa katika nchi Tatu ambazo ni Tanzania,Uganda na Ethiopia ambapo walegwa wakuu wakiwa ni watoto wa wakimbizi waliopo katika kambi za wakimbizi.