Chato, Geita
Madaktari bingwa wa mifupa, ubongo, mgongo na mishipa ya fahamu kutoka Taasisi ya Tiba ya Mifupa na Ubongo Muhimbili (MOI), wakishirikiana na wenzao wa Hospitali ya Rufaa ya Kanda Chato (CZRCH), wamefanikiwa kwa mara ya kwanza kufanya upasuaji mkubwa wa kuondoa uvimbe kwenye ubongo (brain tumor). Upasuaji huo umefanyika kwa mtoto wa miaka tisa aliyekuwa na uvimbe katika pande zote mbili za ubongo, hali iliyosababisha kupooza mikono na miguu pamoja na kupoteza fahamu.
Upasuaji huu ni sehemu ya kambi ya matibabu ya magonjwa ya mifupa, ubongo, na mishipa ya fahamu, iliyozinduliwa mapema mwezi huu, Novemba 4, 2024, na Katibu Tawala Mkoa wa Geita, Bw. Mohamed Gombati, katika Hospitali ya Rufaa ya Kanda Chato.
Dkt. Alpha Kinghomella, Daktari Bingwa Mbobezi wa Ubongo kutoka MOI, amesema:
“Tumefanikiwa kumfanyia upasuaji mtoto huyu baada ya kugundua uvimbe katika pande zote mbili za ubongo, hali iliyomfanya apoteze uwezo wa kujitambua na kupooza mikono na miguu. Tumeondoa uvimbe upande mmoja na kuchukua sampuli kwa ajili ya vipimo zaidi. Mtoto kwa sasa ameanza kujitambua na kuzungumza, na ataendelea kuwa chini ya uangalizi wetu kwa matibabu zaidi.”
Kufikia sasa, zaidi ya wananchi 200 wamepata huduma za matibabu, huku wagonjwa 7 wakifanyiwa upasuaji mkubwa wa ubongo, magoti, na pingili za mgongo. Zoezi la matibabu haya maalumu linaendelea kutolewa na madaktari bingwa wa MOI katika hospitali hiyo, na ni endelevu.
Hospitali ya Rufaa ya Kanda Chato imeendelea kuwa kitovu muhimu cha huduma za afya za kibingwa katika mikoa ya kanda ya Ziwa, ikiwa ni sehemu ya juhudi za serikali kuboresha huduma za afya kwa wananchi wa mikoa hii.