Makamu Mkuu wa Chuo cha Afya na Sayansi Shirikishi Cha Mhimbili Muhas, Profesa Apolinary Kamuhabwa (kulia) na Mkurugenzi wa Kampuni ya ujenzi ya Mohamed Building LTD, Taher Jafferji, wakibadilishana Mkataba baada ya kusaini makubaliano ya ujenzi wa Ndaki ya Tiba katika Kampasi ya Mloganzila kupitia mradi wa Elimu ya juu kwa mageuzi ya Kiuchumi(HEET project) wenye thamani ya shilingi bilioni 50.
Mratibu wa Mradi wa Elimu ya Juu kwa Mageuzi ya Uchumi (HEET) Prof. Erasto Mbughi akizungumza wakati wa utiwaji saini wa mikataba wa ujenzi wa Ndaki ya Tiba kati ya wakandarasi M/S Mohamed Builders na M/S Hainan International Ltd katika Kampasi ya Mloganzila kupitia mradi wa Elimu ya juu kwa mageuzi ya Kiuchumi(HEET project) wenye thamani ya shilingi bilioni 50.
Mkuu wa Wilaya ya Ubungo, Hassan Bomboka akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, wakati wa utiwaji saini wa mikataba wa ujenzi wa Ndaki ya Tiba kati ya wakandarasi M/S Mohamed Builders na M/S Hainan International Ltd katika Kampasi ya Mloganzila kupitia mradi wa Elimu ya juu kwa mageuzi ya Kiuchumi(HEET project) wenye thamani ya shilingi bilioni 50.
Mkuu wa Wilaya ya Ubungo, Hassan Bomboko wa kwanza kulia, Harrison Mwakyembe Mwenyekiti wa Bodi ya Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS) wa katikati na Prof. Erasto Mbughi wakifuatilia tukio la utiwaji saini wa mikataba wa ujenzi wa Ndaki ya Tiba kati ya wakandarasi M/S Mohamed Builders na M/S Hainan International Ltd katika Kampasi ya Mloganzila kupitia mradi wa Elimu ya juu kwa mageuzi ya Kiuchumi(HEET project) wenye thamani ya shilingi bilioni 50.
Na Karama Kenyunko Michuzi Tv
CHUO Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi (MUHAS), kimesaini mkataba wenye thamani ya sh. bilioni 50 na makampuni mawili kwa ajili ya kujenga miundombinu ya kufundishia na kujifunzia katika kampasi ya Mloganzila na Kigoma.
Tukio la kusaini mkataba huo limehudhuriwa na Mkuu wa Chuo cha MUHAS, Prof. Apolinary Kamuhabwa, pamoja na wawakilishi wa makampuni ya Mohamed Builders, Hainan International Ltd, na Mwenyekiti wa Bodi ya MUHAS, Dkt. Harrison Mwakyembe.
Akitoa muhtasari wa mradi huo, Prof. Erasto Mbughi ambaye ni Mratibu wa mradi wa Elimu ya juu kwa Mageuzi ya Uchumi (HEET) chuoni hapo , amesema kuwa ujenzi huo utakuwa kwa kipindi cha miezi 18.
“Leo tunasaini mikataba ya ujenzi wa miundombinu ya kufundishia katika Chuo chetu , mikataba hii inathamani ya shilingi Bilioni 50 miktaba hii ni sehemu ya utekelezaji wa mradi wa elimu ya juu kwa mageuzi ya uchumi (HEET), amesema Prof. Mbughi.
Amesema kuwa mradi huo unaodhaminiwa na Serikali ya Tanzania kupitia fedha za mkopo kutoka Benki ya Dunia (WB) na utasimamiwa na MS Mohamed Bulders Ltd na na M/S Hainan International Ltd.
Amesema kuwa mradi umegawanywa katika sehemu kuu mbili: ya kwanza yenye thamani ya shilingi bilioni 23.4 za Kitanzania itahusisha ujenzi wa jengo la utawala, maktaba, vituo vya ICT, pamoja na miundombinu ya ziada kama uwanja wa soka na njia za kupita kwa miguu.
Sehemu ya pili, yenye thamani ya zaidi ya bilioni 26.7, itajikita katika ujenzi wa madarasa, maabara, hosteli, na cafeteria.
Prof. Mbughi amesisitiza kuwa kukamilika kwa kampasi hii mpya ya matibabu kutakuwa na mchango mkubwa katika kutatua changamoto ya uhaba wa wataalamu wa afya kwa kuongeza uwezo wa MUHAS.
“Chuo chetu ni miongoni mwa taasisi 23 zinazonufaika na mradi huu wenye thamani ya shilingi Bilioni 120” amesema.
Mradi wa HEET ulianza Julai 13, 2021 na unatarajiwa kukamilika Julai 31, 2026.
Naye Mkuu wa Wilaya ya Ubungo Hassan Bomboko, amesema kuwa ujenzi huo utatoa tija kwa Tanzania kuzalisha wataalam katika sekta ya ya afya.
“Mwaka 1963 kulianzishwa chuo cha Muhimbili, hii ilikuwa ni miaka miwili baada ya kupata uhuru lakini mwaka mmoja kabla ya Muungano mnaweza mkaona ni kitambo kirefu sana lakini leo tumekutana hapa ni jambo la kumshukuru mungu kwa sisi sote tuliokuwepo hapa kuwa sehumu ya historia baada ya miaka mingi leo tunakwenda kuona zoezi kubwa linalokwenda kugharimu zaidi Bilioni 50 ambalo linakwenda kuweka histori …jambo hili ni kubwa sana” amesema DC Bomboko.
Aidha amempongeza Rais Samia kwa kuwekeza kwenye sekta ya afya
“Nimpongeze Rais Dk. Samia kwa kuwa na ‘Political Will yapo maeneo mengi sana ambayo angeweza kuwekeza lakini alipopata mkopo huu amemua kuwekeza kwenye sekta ya afya hii ni dhamira ya kweli na ya dhati ya Rais Samia ya kuhakikisha analinda nguvu kazi ya taifa letu kwa kutengeneza waataalam hapa tunaenda kutengeneza mkataba wa ujenzi wa kiwanda cha kuandaa wataalam wa sayansi ya tiba leo”
Amesema kuwa ujenzi huo kama Rais Samia asingekuwa na maono kwenye maendeleo ya Sekta ya Afya pesa hizo asingezipeleka kwenye miradi hiyo ” ameweza kuhakikisha miradi hii inaleta tija kwenye elimu ya juu “
Kwa upande wake, Mkuu wa Chuo cha Muhas Prof. Appolinary Kamuhabwa, ameishukuru serikali kwa kuwapa kipaumbele na kuwawahimiza wakandarasi kuhakikisha kuwa mradi unatekelezwa kwa thamani ya fedha na unakamilika kwa wakati akibainisha kuwa wakandarasi walichaguliwa kutokana na uwezo wao.
“Tunaishukuru sana Serikali kwa kukipa chuo hiki kipaumbele katika mradi huu ambao tunaamini utatoa matokea mazuri kwenye sekta ya afya hususan katika Teknolojia ya matibabu”. Amesema Prof. Kamuhabwa