Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Philip Mpango, anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika Kongamano la Tatu la Kimataifa la Kisayansi linaloandaliwa na Taasisi ya Utafiti wa Misitu Tanzania (TAFORI). Kongamano hilo litafanyika jijini Arusha kuanzia tarehe 11 hadi 13 Desemba 2024, likilenga kujadili mbinu za kurejesha mandhari ya misitu kwa maendeleo endelevu na kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.
Kongamano hilo la siku tatu litafanyika katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Arusha (AICC) chini ya mada kuu: “Kurejesha Mandhari ya Misitu kwa Maendeleo Endelevu na Kukabiliana na Mabadiliko ya Tabianchi” (Restoring Forest Landscapes for Sustainable Development and Climate Change Mitigation).
Akizungumza kuhusu kongamano hilo, Mkurugenzi Mkuu wa TAFORI, Dkt. Revocatus Mushumbusi, amesema linatarajiwa kuwakutanisha zaidi ya washiriki 400 kutoka ndani na nje ya nchi. Washiriki hao ni pamoja na wanasayansi, watunga sera, wanaharakati wa mazingira, wawakilishi wa vyuo vikuu, wapanda miti, na wadau wengine wa sekta ya misitu na ufugaji nyuki.
Dkt. Mushumbusi ameainisha kuwa kongamano hilo linalenga kuwakutanisha wataalam wa sekta ya misitu na ufugaji nyuki ili kujadiliana, kubadilishana uzoefu, na kuwasilisha matokeo ya tafiti mbalimbali kuhusu usimamizi endelevu wa maliasili. Aidha, linatarajiwa kuibua miradi mipya ya uhifadhi na mbinu bora za kurejesha misitu kwa maendeleo endelevu.
Mbali na hayo, kongamano hili pia litakuwa sehemu ya maandalizi ya Mkutano Mkuu wa Wafugaji Nyuki Duniani (APIMONDIA) unaotarajiwa kufanyika nchini Tanzania mwaka 2027.
Dkt. Mushumbusi ametoa wito kwa wadau wote wa sekta ya misitu na ufugaji nyuki kushiriki kikamilifu kwa kusajili majina yao kupitia tovuti rasmi ya TAFORI: www.tafori.or.tz. Viingilio vya ushiriki ni:
TSh 200,000 kwa wadau wa Afrika Mashariki,
TSh 100,000 kwa wanafunzi, na
TSh 350,000 kwa wadau kutoka nje ya Afrika Mashariki.
Kongamano hili ni fursa muhimu ya kuimarisha juhudi za pamoja za kukabiliana na changamoto za mazingira na kukuza maendeleo endelevu nchini na kimataifa.