#Wananchi wahamasishwa kutunza miundombinu ya barabara
Babati, Manyara
Wakala ya Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) Mkoa wa Manyara ina mpango wa kufungua barabara mpya zenye urefu Km. 109 katika Wilaya ya Mbulu, Simanjiro pamoja na Babati katika mwaka wa fedha 2024/2025.
Hayo yamebainishwa na Kaimu Meneja wa TARURA Mkoa wa Manyara Mhandisi Salim Bwaya wakati akiongea na waandishi wa habari mkoani hapo.
Mhandisi Bwaya amesema kwamba kilomita hizo za barabara zinaenda kuwanufaisha wananchi na kuwaletea manufaa kiuchumi na kuwarahisishia kupata huduma za kijamii kwa urahisi.
“Mwaka huu wa fedha tuna mpango wa kufungua barabara katika wilaya ya Mbulu (Km. 46), Simanjiro (Km. 41), pamoja na Babati (Km. 22) ambapo itajumuisha ujenzi wa barabara za lami(Km. 11.7),changarawe (Km. 251.4) pamoja na matengenezo ya barabara za udongo (Km. 385) na ujenzi wa vivuko vipatavyo 104,” amesema.
Amesema kwamba licha ya kufungua kilomita hizo za barabara hali ya upitikaji wa barabara maeneo mengi ya barabara hizo hupitika kipindi chote cha mwaka.
Aidha, amesema kuwa utekelezaji huo unaendelea kutokana na ongezeko la bajeti katika mkoa huo ambapo kwa sasa bajeti yao imepanda mara tatu kutoka Shilingi bilioni 6.788 mwaka 2021 hadi kufikia Shilingi bilioni 19.7 mwaka 2024/2025
“Hii ni ongezeko kubwa na kutufanya tuongeze ubora wa mtandao wetu wa barabara kwa miaka ya 2021 tulikuwa na barabara za lami Km. 17 na sasa tuna Km. 33.03, barabara za changarawe kutoka Km. 950 hadi kufikia Km. 1980 na kiwango kinachobaki ni kiwango cha udongo”.Aliongeza.
“Tunaishukuru Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kutuongezea bajeti mara tatu ya bajeti ya awali na hivyo tumeweza kuongeza madaraja ya mawe kutoka daraja (1) mwaka 2021 hadi kufikia madaraja (10),”.
Pia amesema wameweza kuongeza madaraja madogo na ya kati kutoka 283 hadi 530 vile vile madaraja makubwa yameongezekwa kutoka madaraja (2) mwaka 2021 hadi kufikia madaraja (28) kwa mwaka huu wa fedha.
Kwa upande wa mabadiliko ya tabia nchi Mhandisi Bwaya amesema kwamba wanaendelea kutoa elimu kwa jamii kuhusu madhara yanayosababishwa na uharibifu wa miundombinu hasa mifereji, kung’olewa kwa alama za barabara na uvamizi wa hifadhi za barabara kwa shughuli za kiuchumi pamoja na umuhimu wa kupanda miti na kutunza mazingira na kuacha kufanya shughuli zingine za kibinadamu kwenye hifadhi za misitu na kwenye vyanzo vya maji.
Hata hivyo ametoa wito kwa wananchi kuendelea kutunza miundombinu ya barabara kwa kuzingatia sheria na kanuni zake kwani Serikali inawekeza fedha nyingi kwenye miundombinu ya barabara hivyo ni wajibu wao kuitunza ili waendelee kunufaika nayo.
Naye, Mkazi wa Babati Bw. Bakari Sanka amesema Mkoa wao unapokea mazao mengi kutoka vijijini hivyo kukamilika kwa ujenzi wa madaraja na miundombinu mingine imewanufaisha wananchi wengi na hivyo shughuli zao za uzalishaji zinaendelea kama kawaida.
Pia Bi. Hadija Shabani amesema wamefurahi sana kwa ujenzi wa madaraja katika kata zao kwani makorongo yalikuwa mengi na hivyo msimu wa mvua wanafunzi na watoto walikuwa wakipata shida kuvuka ila kwa sasa imewaokoa na kuwarahisishia usafiri.