…………….
Na Hellen Mtereko,Mwanza
Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Said Mtanda amezindua tamasha la Ilemela nyama choma litakalokuwa likifanyika kila jumamosi katika viwanja vya Nanenane.
Uzinduzi huo umefanyika Leo Jumamosi Novemba 16, 2024 katika viwanja vya Nanenane vilivyoko Kata ya Nyamhongoro Wilaya ya Ilemela Mkoani Mwanza.
Akizungumza kabla ya uzinduzi huo Mtanda, alisema tamasha hilo litakuwa na faida nyingi ikiwemo ya kuchochea uchumi wa mtu mmoja mmoja na taifa kwa ujumla.
Pia aliongeza kuwa tamasha hilo litasaidia kuongeza mapato ya Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela pamoja na kuimarisha mahusiano.
“Tamasha hili ni fursa nzuri kwa wakazi wa Mwanza kwani litawakutanisha watu mbalimbali na litaimarisha uchumi wao”, Alisema Mtanda
Aidha, aliwaomba wadau wa nyama choma kuendelea kutoa ushirikiano kwenye Ofisi ya Mkurugenzi kwakutoa ushauri utakaosaidia kuboresha tamasha hilo.
Kwaupande wake Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela, Ummy Wayayu alisema tamasha hilo litasaidia kujenga afya za watu kwani sasa hivi watu wanamsongo wa mawazo.
Alisema kadri siku zitakavyoenda watazidi kuboresha tamasha hilo kwakuweka mashindano ya kuchoma nyama,kupiga Ngoma na bendi za muziki.
Naye Mbunge wa Jimbo la Ilemela Dkt.Angeline Mabula, aliwaomba waandaaji wa tamasha hilo kuwa wabunifi katika uchomaji wa nyama sanjari na kuleta aina mbalimbali za nyama.
Awali akizungumza kwenye tamasha hilo Katibu wa wadau wa nyama choma Ezra Shandu, aliomba miundo mbinu iboreshwe ili biashara ziweze kufanyika vizuri hususani katika kipindi hiki cha mvua hatua itakayosaidia kulinda vifaa vyao vya kazi.
Aliongeza kuwa majadiliano ya maboresho yanapofanyika wahusishwe ili kufanya zoezi hilo kuwa na mvuto zaidi kwani wao ndio wanawajua wateja wao vitu wanavyohitaji.