Na Mwandishi Wetu
Benki
ya NMB imedhihirisha tena ukubwa wake nchini, baada ya mwaka huu kuweka
rekodi kwa kutwaa zaidi ya tuzo 30 zinazotambua ubora wa huduma zake,
ubunifu, ufanisi katika uendeshaji na utendaji, pamoja na mchango wake
mkubwa katika ujenzi wa taifa.
Mafanikio
hayo ya kipekee kitasnia na makubwa kitaifa na kimataifa yalibainishwa
jana jijini Mwanza na Afisa Mtendaji Mkuu, Bi Ruth Zaipuna, katika
mkutano wa viongozi wakuu wa benki hiyo pamoja na mameneja wa matawi
yake zaidi ya 240.
Akizungumza
pembezoni mwa mkutano huo, Bi Zaipuna alisema ushindi huo ni hatua kubwa
kwao inayotokana na juhudi za wafanyazi pamoja na uwekezaji unaofanyika
katika teknolojia za kisasa na kubuni masuluhisho ya kuwahudumia wateja
na taifa kwa ujumla.
“Mwaka huu
tumeshinda zawadi mbalimbali na tuzo zaidi ya 30 za kitaifa na kimataifa
zikiwemo zile za Benki Bora Tanzania kwa Mwaka 2024, kutoka jarida la
Euromoney; Ubunifu Bora katika Huduma za Kibenki kwa Wateja Binafsi
kutoka International Banker Magazine; na Benki Bora Huduma Ujumuishi za
Kifedha 2024 ya jarida la World Economic Magazine,” alimwambia mgeni
rasmi wa mkutano huo, Mkuu wa Wilaya ya Kwimba, Bw Ng’wilabuzu Ludigija.
Aidha,
alimueleza kiongozi huyo kuwa kwa mara 11 mfululizo katika miaka 12,
NMB imekuwa ikitwaa tuzo ya benki bora na kuwa ushahidi wa umahiri wake
wa ubunifu ni masuluhisho mpya inayoyatambulisha sokoni kila kukicha na
mfano mzuri wa hilo ni huduma ya NMB Jiwekee iliyoanza mwaka huu.
Upande
wa ujumuishaji kifedha, Bi Zaipuna alisema kupitia Mkakati wa Benki
Vijijini, wanatarajia mwakani kuhakikisha kila kijiji nchini kinafikiwa
na huduma za kifedha. Mchakato huu, aliongeza, unachangia pia kufanya
sekta isiyo rasmi kuwa sehemu ya uchumi rasmi na kusaidia kupanua wigo
wa kodi nchini.
“Pia tunafanya vizuri
upande wa usawa wa kijinsia mahala pa kazi na kufadhili jitihada za
kuwakwamua kifedha na kuwawezesha kiuchumi akina mama, kwa hiyo
tumeshinda pia tuzo kadhaa katika eneo hili,” iliongeza na kusema kwa
sasa asimilia 48 ya wafanyakazi wote wa NMB ni wanawake na waliobaki
asilimia 52 ni wanaume.
Tuzo
ilizoshinda NMB mwaka huu zinahusiana na masuala ya kijinsia ni pamoja
na kuibuka Mshindi wa Jumla – Afrika Mashariki: Kiongozi wa Usawa wa
Kijinsia. Nyingine ni ile ya Uwezeshaji ya Wanawake Mahala pa Kazi, Tuzo
ya Taasisi Inayoongoza Uwekezaji kwa Vijana wa Kike pamoja na Nishani
ya Fedha – Mfadhili Mahiri wa Wajasiriamali Wanawake.
Majarida
mengine ya kimataifa na taasisi za ndani nan je zilizoitunuku tuzo NMB
mwaka huu ni pamoja na Global Banking & Finance Awards® Review,
Global Business Magazine, International Business Magazine, Global Brands
Magazine, na Shirika la IFC na Soko la Hisa la Dar es Salaam (DSE)>
“Mwaka
huu tumepokea tuzo zaidi ya 30 za kitaifa na kimataifa na hii ni hatua
kubwa sana na tuna kila sababu ya kupongezana kwa hili,” Bi Zaipuna
aliwaambia wajumbe wa mkutano huo ambao ufanyika kila mwishini mwaka
kutathimini utendaji na kuweka mikakati.
“Nitumie
nafasi hii kuwapongeza wafanyakazi wote wa Benki ya NMB kote nchini kwa
kufanya kazi kwa uadilifu, bidii, juhudi na maarifa, hali
iliyotupelekea kuaminika na taasisi kubwa duniani na kututambua kama
benki bora katika maeneo takribani yote.”
Tuzo
nyingine ilizozinyakua NMB mwaka huu ni pamoja na ile ya Benki Bora ya
Kidijitali, Benki Bora kwa Uwekezaji Tanzania, Benki Bora ya Wateja
Binafsi na Biashara, na Tuzo ya Afisa Mtendaji Mkuu Bora kwa Mabenki
nchini Tanzania.
Orodha hii
inajumuisha pia tuzo za Benki Bora kwa Wateja Wadogo 2024, Mtunza Mali
Bora wa Mwaka, Mtoa Hati Fungani Bora, Benki Bora kwa ESG inayohusiana
na mambo ya mazingira, jamii na utawala bora, pamoja na tuzo za ubora na
ubunifu wa hatifungani ya NMB Jamii Bond.
“Mwaka
huu, Benki ya NMB tumeshinda pia tuzo ya Kampuni Bora Iliyoorodheshwa
Soko la Hisa la Dar es Salaam kwa upande wa mabenki,” Bi Zaipuna alisema
na kuongeza kuwa kabla ya mwezi Mei walikuwa pia wameshinda tuzo za
Benki Bora ya Wateja Maalum na Benki Bora ya Wateja Wenye Mali.
“Pia
tumepokea tuzo ya Benki Bora ya Mikopo na Miradi ya Mkakati na Best
Trade Finance Bank Tanzania 2024 kutoka kwa International Business
Magazine pamoja na Best Trade Partner Bank – Advisory Services 2024
kutoka kwa International Finance Corporation (IFC),” iliongeza.
Kwa
upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Kwimba, Bw Ludigija, aliipongeza NMB kwa
mafanikio makubwa inayoendelea kuyapata na kuchangia katika ujenzi wa
taifa na maendeleo ya nchi kwa ujumla.
Aliuambia
mkutano huo kuwa uwepo wa benki hiyo katika kila eneo nchini kunaifanya
kutegemewa na Watanzania karibu wote hata wale wanaoishi vijijini
pamoja na viongozi wa ngazi zote kutokana na kushirikiana kwake kwa
karibu na Serikali.
Bw
Ludigija ameiomba NMB kuendelea kuchangia maendeleo mkoani Mwanza na
hususan wilaya ya Kwimba akisema mkoa huo una utajiri mkubwa wa mazao ya
kilimo na samaki pamoja na madini.