Mahafali ya 23 ya Chuo cha Bandari Dar es Salaam yatafanyika Ijumaa Desemba 06 2024 katika Viwanja vya Chuo hicho huku Mgeni Rasmi akitarajiwa kuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Uchukuzi Prof. Godius Kahyarara.
Akitoa taarifa ya Mahafali kwa Waandishi wa Habari, Mkuu wa Chuo hicho Dkt. Lufunyo Hussein amesema, Wahitimu 794 wa ngazi ya Astashaha na Stashahada watatunukiwa Vyeti vyao baada ya kuhitimu na kufaulu mafunzo yanayotolewa na Chuo hicho.
Kuhusu mipango ya baadae ya Chuo, Dkt. Lufunyo amesema, Chuo kinachukua hatua za kimkakati za kuboresha mitaala yake ili kukidhi mahitaji ya sasa ya Sekta ya Bandari na mabadiliko mbalimbali yanayojitokeza ikiwemo uamuzi wa Serikali kushirikiana na Sekta binafsi katika kuendesha na kuendeleza Sekta ya Bandari Nchini.
Aidha, Chuo cha Bandari kinatoa mafunzo ya Weledi na Umahiri wa kuhudumia miradi ya utafutaji wa Mafuta na Gesi na mafunzo ya uendeshaji na utengenezaji wa mashine na mitambo mbalimbali ya kutolea huduma katika Bandari na Bandari Kavu.