

Amesema wataalam wa ununuzi na ugavi ni muhimu katika kuchagiza maendeleo na Serikali inawategemea ili kufanikisha mipango yake.
“ Wataalam wa manunuzi na ugavi mna mchango mkubwa, zaidi ya
asilimia 70 ya bajeti nzima ni kwa ajili ya manunuzi, hivyo kuweni waadilifu, Chukieni Rushwa na kushauri namna bora ya kufanikisha mipango ya Maendeleo” amesema Dkt. Biteko.
Amesema kutokana na ukubwa wa majukumu yao kuna uwezekano rushwa kubwa ikapita mikononi mwao, hivyo majadiliano haya yawawezeshe kuzuia na kukabiliana na vitendo hivyo.

Hata hivyo, Dkt. Biteko amewataka washiriki wa Kongamano hilo kujifanyia tathimini kuhusu utendaji wao wa kazi ili kuondokana na Changamoto zinazoweza kuichafua taaluma ya ununuzi na ugavi.
“ Zipo sauti nanyi mnazisikia, ili uweze kupata tenda lazima kuwa na urafiki na Afisa ununuzi, wanasema ukifuata taratibu za ununuzi gharama zinaongezeka zaidi ya kawaida, wengine wanasema siri za tenda zinapatikana miongoni mwa watumishi, wengine wanalaumu na wengine wanasifia, Jambo la msingi sikilizeni sauti za watu na mjitathimini,” amesisitiza
Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Fedha, Mhe. Hamad Chande amewataka washiriki kufanya kazi zao kwa kushirikiana huku Wizara yake ikiendelea kutafuta suluhisho la changamoto zinazowakabili wataalam wa ununuzi na ugavi.
Amesema miongoni mwa mambo yanayosababisha mkwamo Serikalini ni pamoja na Wivu, choyo na fitna miongoni mwa watumishi, hivyo amewataka kuondokana na mambo hayo ili kukua na kujiletea maendeleo.
“Sheria ya ununuzi wa umma sura 410 inawalinda wataalam wa ununuzi na ugavi hivyo watembee kifua mbele na kuhakikisha wanafanya kazi kwa mujibu wa sheria zilizopo”.
Makamu Mwenyekiti wa Bodi ya Wataalamu wa Ununuzi na Ugavi (PSPTB) Benezeth Ruta ameishukuru Serikali kwa kutenga fedha zinazoiwezesha taaluma hiyo kusonga mbele.
Amesema Bodi hiyo inaendelea na utekelezaji wa Sheria Na. 23 ya mwaka 2007 kuhakikisha kuhakikisha Wataalam wanaofanya shughuli za ununuzi na ugavi wana sifa stahiki za kufanya kazi hizo.