Mwandishi Wetu .
Tume
Huru ya Taifa ya Uchaguzi imetangaza ratiba ya uboreshaji wa Daftari la
Kudumu la Wapiga Kura kwenye mikoa ya Ruvuma, Njombe, Songwe na Rukwa
ambapo zoezi hilo litafanyika kwa siku saba kuanzia tarehe 12 hadi 18
Januari, 2025.
Hayo yameanishwa kwenye hotuba ya Mwenyekiti wa
Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi, Jaji wa Mahakama ya Rufaa, Mhe. Jacobs
Mwambegele iliyosomwa kwa niaba yake kwenye mikutano ya Tume na wadau wa
uchaguzi iliyofanyika leo tarehe 31 Desemba, 2024 kwenye mikoa ya
Ruvuma, Njombe, Songwe na Rukwa.
Mhe. Mwambegele ambaye
aliwakilishwa na wakurugenzi mbalimbali wa Tume kwenye mikutano hiyo,
amesema mikoa hiyo itafanya uboreshaji kwenye mzunguko wa tisa na kwamba
tayari Tume imekamilisha uboreshaji kwenye mikoa 19 ambayo ilijumuisha
mizunguko nane kati ya mizunguko 13 ambayo imepangwa kukabilisha zoezi
hilo nchini.
“Leo tupo hapa Songwe na wenzetu wapo kwenye mikoa
ya Njombe, Rukwa na Ruvuma ikiwa ni maandalizi ya uboreshaji wa Daftari
kwenye mkoa huu wa Songwe, Njombe, Rukwa na mkoani Ruvuma kwenye
Halmashauri za Wilaya ya Nyasa, Mbinga, Mbinga Mji, Wilaya ya Songea na
Manispaa ya Songea, zoezi litakalofanyika kwa muda wa siku saba kuanzia
tarehe 12 Januari, 2025 na kukamilika tarehe 18 Januari, 2025 na ambapo
vituo vitakuwa vinafunguliwa kuanzia saa 2:00 asubuhi na kufungwa saa
12:00 jioni,” imesema sehemu ya hotuba hiyo.
Ameitaja mikoa
ambayo tayari imekamisha zoezi hilo kuwa ni Kigoma, Tabora, Katavi,
Geita, Kagera, Mwanza, Shinyanga, Mara, Simiyu, Manyara, Dodoma na
Singida.
“Mikoa mingine ni mikoa ya Zanzibar ambayo ni Mjini
Magharibi, Kusini Unguja, Kaskazini Unguja, Kusini Pemba, Kaskazini
Pemba, Arusha na Kilimanjaro. Kwa sasa mikoa miwili ya Mbeya na Iringa
inatarajia kukamilisha zoezi hilo tarehe 02 Januari, 2025,” imesema
sehemu ya hotuba hiyo.
Mada ya Mkurugenzi wa Uchaguzi, Bw.
Kailima Ramadhani iliyowasilishwa kwa niaba yake kwenye mikutano hiyo
imeanisha kwamba kwenye mikoa hiyo jumla ya wapiga kura wapya 475,743
wanatarajiwa kuandikishwa kwenye Daftari la Kudumu la Wapiga Kura.
Mada
hiyo imeanisha kuwa uboreshaji wa Daftari utakapokamilika, mikoa hiyo
inatarajiwa kuwa na jumla ya wapiga kura 3,091,485 ikilinganishwa na
idadi ya wapiga kura 2,615,742 waliokuwemo kwenye Daftari mwaka 2020.
“Idadi
hii inaweza kuongezeka kwa kuwa inawezekana wapo watanzania ambao
walikuwa na sifa za kuandikishwa kuwa wapiga kura wakati wa uboreshaji
wa Daftari mwaka 2019/20, lakini kwa sababu moja au nyingine hawakuweza
kujiandikisha,” imesema sehemu ya mada hiyo.
Mada hiyo imeanishwa kuwa kutakuwa na vituo 3,785 ikiwa ni ongezeko la vituo 233 kutoka vituo 3,552 vilivyokuwepo mwaka 2020.