Na Said Mwishehe,Michuzi TV
Mimi
Said Mwishehe kwanza kabisa kwa kipekee naomba nimshukuru Muumba wa
mbingu na ardhi kwa kutujaalia afya na uzima na leo tuko mwaka 2025,
Tumevuka mwaka salama kwa uwezo wake maanani.
Tunafahamu mwaka
2024 ulikuwa mwaka wenye mafanikio na changamoto zake lakini tumevuka na
sasa tunaaanza safari ya mwaka 2025.Tumuombe Mungu atuweke, atupe afya
njema na uhai tuumalize mwaka 2025, Tuseme Inshallah.
Baada ya
utangulizi huo wa salamu naomba pia niendelee kuwashukuru na kuwapongeza
Watanzania wenzangu kwa kuendelea kuwa wamoja na kuhakikisha
tunasimamia misingi iliyowekekwa na waasisi wa taifa hili na hasa suala
la zima la kutunza amani ya Nchi yetu .
Pia najua mwaka 2024
ulikuwa ni mwaka wa kufosi na kuna Msanii mmoja wa bongo Fleva katika
sehemu yake ya Mashairi mbali ya kusema huu ni mwaka wa kufosi akaenda
mbali zaidi kwamba lazıma watamuita bosi, hivyo ni wakati wa kutafakari
kuwa tumefosi na kuitwa bosi au tumekwama?Tujipange mwaka 2025 naamini
kila kitu kitakaa sawa, acha uoga.
Naomba nirejee katika hoja
yangu ya msingi ambayo inanifanya niandike salamu zangu za mwaka 2025
kwa Rais Dk.Samia Suluhu Hassan pamoja na Chama Cha Mapinduzi(CCM)
ambacho wewe ni Mwenyekiti wake Taifa.
Rais wangu Dk.Samia Suluhu
Hassan, Nakusalimu kwa jina la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, baada
ya salamu hiyo na baada ya kujibu Kazi Iendelee naomba niseme mapema
kabla ya kukuchosha, Naomba nikupongeze kwa kazi kubwa na nzuri
unayoendelea kuifanya ya kuwatumikia Watanzania.
Tangu umekuwa
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania umeonesha uzalendo mkubwa katika
kulitumikia Taifa la Tanzania,umekuwa Rais mwenye upendo,huruma kwa
wananchi unawaongoza na kubwa zaidi umekuwa msikivu,hongera Rais Samia.
Uongozi
wako umekuwa ukitanguliza zaidi hekima na busara katika kufanya maamuzi
yako kwa ajili ya nchi yetu,hakika uongozi wako unaifanya Tanzania kuwa
katika mikono salama,hakika tunajivunia uongozi wako.Dk.Samia wewe ni
Rais, wewe ni Mama yetu.Upendo wako unaishi katika mioyo yetu.
Nakumbuka
wakati unachukua kijiti cha uongozi kutoka kwa mtangulizi wako Hayati
Dk.John Pombe Magufuli, ulituhakikishia Watanzania kuwa nchi iko katika
mikono salama.Wenye mashaka na wewe uliwaambia wasiwe na wasiwasi nchi
itakwenda,miradi yote itatekelezwa na kukamilika na utaanzisha miradi
mingine.
Hakika mimi na Watanzania wenzangu tumeshuhudia kazi
kubwa ambayo umeifanya na unayoendelea kuifanya kwa kuhakikisha miradi
ya maendeleo inaendelea kutekelezwa.
Rais Samia naomba upokee
salamu zangu za kukutakia heri ya mwaka mpya wa 2025.Nakuombea afya
njema,nakuombea uendelee kuwa mwenye hekima na busara katika
uongozi.Tunajivunia uongozi wako.Nchi imetuliaa hadi raha.
Wakati
unachukua Nchi wapo baadhi ya watu walikuwa wanakuchukulia poa,
walidiriki kusema hutaweza,hutaweza kutekeleza miradi.Leo hii wale watu
wamefunga midomo,waliko wanaona aibu.Kazi kubwa ambayo umeifanya kwa
kweli kwa lugha ya watoto wa mwaka 2000 ni kwamba umewanyoosha.Wametulia
huko waliko.
Wakiangalia bwawa la kuzalisha umeme la Mwalimu
Nyerere kazi imefanyika na umeme umeunganishwa katika gridi ya
Taifa,tumeanza kuonja utamu wa Mradi wa bwawa la Mwalimu Nyerere.Naamini
mradi utakapokamilika kwa mitambo yote kufanya kazi kwa asilimia 100
mbona tutajibweda,tutajinoma sana.
Mradi wa reli ya kisasa kwa
ajili ya treni ya umeme maarufu kama SGR wote ni mashahidi,kutoka Dar es
Salaam kwenda Morogoro na Dar es Salaam kwenda Dodoma sasa tunajidai
tu. Unalala Dodoma chai unakuja kunywa Dar.
Nakupongeza Rais
Samia kwa kusimamia vema Mradi wa reli ya SGR, nafahamu kazi ya Ujenzi
kutoka Dodoma kwenda Mwanza na baadae Kigoma kazi inakwenda vizuri
sana,unastahili pongezi Rais Samia.Wale ngedere wanaokata umeme na
kuharibu miundombinu ya SGR najua chini ya uongozi wako dawa yao iko
jikoni.
Najua kazi kubwa na nzuri ambayo unaifanya Rais Samia
katika Nchi yetu,miradi ya miundombinu ya barabara imeendelea kuboreshwa
chini ya Serikali unayoingoza, kwa Dar es Salaam barabara za mwendo
kasi unaendelea kuzijenga na umegusa barabara zote muhimu.
Miradi
ya barabara hizo ukikamilika Dar itakuwa tamu mnoo.Najivunia kuwa na
Rais Samia.Ujenzi wa miundombinu ya barabara unaifanya katika kila kona
ya nchi yetu,Watanzania ni mashahidi.
Hata hivyo Rais Samia
wakati natuma salamu hizi za mwaka mpya kwako naomba nikukumbushe wakazi
wa Majohe Kwasoma walioko katika Jimbo la Ukonga Jijini Dar es Salaaam
tunakuomba barabara ya lami , nafahamu kipande cha urefu wa mita 200
tumewekewa lami na vitaa vya juu.
Kuwekwa lami kwa kipande hicho
kidogo sana kunaashiria barabara ya kutoka Sekondari ya Pugu kwenda
Majohe Kwasoma,Halisi hadi kwa Mpemba tutapata lami katika mwaka huu wa
2025, ndio kılio chetu kikubwa wakazi wa Majohe Kwasoma.
Ikikupendeza
Rais wangu tusaidie lami katika barabara yetu ya Majohe Kwasoma hadi
kwa Mpemba kwani utakuwa umetatatua changamoto kubwa ya usafiri halafu
kuhusu tunakula na kuvaa nini hilo tuachie wenyewe.
Ngoja
tuachane na ombi la barabara ya lami ya Majohe Kwasoma, nijikite katika
salamu zangu za mwaka mpya kwako Rais Samia, naomba nikupongeze kwa
hatua unazoendelea kuchukua kuboresha sekta ya afya kwa kujenga
miundombinu ya huduma za afya, kununua Dawa na Vifaa Tiba.Umeongeza
bajeti ya sekta ya afya.Bohari ya Dawa (MSD) wameendelea kuboresha
huduma zao.
Katika afya Rais Samia naomba nikwambie tu kama kuna
eneo ambalo binafsi nimefurahishwa ni katika suala la Bima ya Afya kwa
wote, katika eneo mojawapo ambalo Watanzania tunapata changamoto ni
gharama za matibabu ya afya.
Gharama ziko juu na kwa Mtanzania
hasa wa kipato cha chini anashindwa kumudu ndio maana tunaishia kununua
Panado tu, uwezo kwenda hospitalini haupo, Nani anaweza gharama zake?
Kwa
kuliona hilo Rais wetu mpendwa tumeona hatua ambazo umeendelea
kuzichukua zikiwemo za kutoa maelekezo yako kwa Wizara ya Afya kupitia
Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya(NHIF) kuwa na Bima ya Afya kwa
Wote.Tunaona hata mchakato umefika hatua nzuri, tumeanza kuona dalili
njema.
Sasa Watanzania tunakwenda kufurahia huduma za afya
kupitia bima ya afya kwa wote.Kuhusu bima ya afya kwa watoto Rais umetoa
maelekezo yenye busara kwa NHIF na sasa watoto wakiwemo wanafunzi
wamerejeshea kifurushi cha Toto Afya Kadi.
Kiiliondolewa hapo
katikati na kuwababisha malalamiko lakini Rais umekirudisha na hii
inathibitisha upendo wako mkubwa kwa watoto wa Taifa hili.Hongera kwa
juhudi zako katika sekta ya afya.Hupendi kusifiwa lakini naomba
uniruhusu nikusifu maana unastahili.
Katika eneo la utunzaji
mazingira Rais Samia pamoja na hatua mbalimbali ambazo Serikali yako
imeendelea kuchukua tunashuhudia mkazo ambao umeuweka katika kuhamasisha
matumizi ya nishati safi ya kupikia, sasa ni mwendo wa gesi tu na muda
si mrefu mkaa na kuni vinakwenda kubaki kuwa historia.
Wananchi
wanatunza mazingira na wakati huo huo wanatunza na afya zao.Nani
anapenda kuwa na macho mekundu kwasababu ya moshi wa kuni ?Tunakushukuru
Rais Samia na ni matumaini yangu hamasa ya nishati safi itaendelea
kuelekea 2032 kama ambavyo umeelekeza.
Rais Samia naomba wakati
unasoma salamu hizi utambue kuwa Watanzania tunakupenda, tunajivunia
uongozi wako ambao umetufanya tuwe na amani ya moyo, hakuna mwenye
presha na watu wanaendelea na shughuli za utafutaji kwa utulivu kabisa.
Hakuna
mwenye wasiwasi ,watu wametulia na maisha yanakwenda.Walioko maofisini
na hasa watumishi wa Umma wanatekeleza majukumu yao bila ya kuwa na
mawazo ya kwamba je itakuaje?Wanaokosea unachukua hatua zinazostahili
bila kuonea mtu.Mungu amekujaalia utu,amekujaalia hekima na busara.
Rais
Samia umeyafanya mengi na hayo ndio ambayo yanafanya niandike salamu
hizi moyo wangu ukiwa na matumaini makubwa na uongozi wako,najua pamoja
na mafanikio makubwa ya uongozi wako kama Taifa tumepitia changamoto ya
baadhi ya watu kupotea.
Kelele zimekuwa nyingi,familia ambazo
zimepotelewa na ndugu ,jamaa na marafiki wamepaza sauti,Watanzania
wametoa vilio vyao katika hili. Hata hivyo hili la watu kupotea
linahitaji mjadala mpana lakini wenye kutuunganisha zaidi na si
kutugawa.
Hata hivyo nikiri nilifurahishwa na maelekezo yako
Rais Dk.Samia Suluhu Hassan kwa vyombo vya ulinzi na usalama kuhakikisha
wanachukua hatua kudhibiti matukio hayo.Umetoa rai kwa Watanzania kutoa
ushirikiano katika kukomesha matukio hayo.
Hivyo wakati natoa
salamu zangu za mwaka mpya kwako natumai utaendelea kutoa maelekezo kwa
vyombo vya ulinzi na usalama kuendelea kuchukua hatua kuhakikisha
matukio ya watu kupotea yanakoma.Hakuna anayefurahishwa na matukio
hayo.Uso wa Rais anapozungumzia watu kupotea umekuwa ukionesha
anavyoumizwa nayo.Pole Rais wetu.
Katika salamu zangu kwako Rais
Samia naomba nikupongeze kwa kazi kubwa ambayo unaendelea kuifanya
katika sekta ya kılımo kupitia Wizara ya Kilimo kwa kushirikiana na
Taasisi zilizopo zinahusika na kilimo.Umeondoa kero ya kuchelewa kwa
pembejeo za kilimo.Umeweka nguvu katika kutafuta Masoko ya mazao yetu,
umeondoa tozo na kodi ambazo zilikuwa kero kwa wakulima.
Rais
Samia Samia kwa sasa kilimo kimekuwa kimbilio la Watanzania walio wengi,
watu wako mjini wanafunga tai shingoni lakini kijijini wanamashamba
,wanalima,wanavuna na kisha wanapiga Pesa.Rais Samia umekuwa na mtazamo
chanya katika kilimo, nafahamu fedha ambazo umeelekeza ziende katika
kujenga miundombinu ya umwagiliaji.
Hakika unastahili
pongezi,nikwambie Rais Samia katika kilimo unaupiga mwingi sana ingekuwa
mchezaji basi nakufananisha na Awesu Awesu maarufu kepteni Lucho fundi
wa boliii.Hapo natania tu kwani wewe ni namba moja kwangu katika kila
kitu kinachohusu nchi yangu nzuri.Hongera Rais Samia ,ipo siku nitakuja
kukusalimia Live Ikulu maana katika ndoto nilishakutana na wewe na
tukazungumza mengi.
Lakini katika sekta ya maji nako tunaona
hatua unazoendelea kuchukua kampeni yako ya kumtua ndoo mama kichwani
imefanikiwa. Maelekezo yako ya maji yawe yanapatikana ndani ya mita 400
yamefanyiwa kazi.Shida ya maji inaendelea kupungua.
Juzi
maelekezo yako baada ya kuona ile video ya mtangazaji wa Clouds TV kule
Tanga nayo imenigusa sana, umeona tatizo na umechukua hatua na leo
wananchi wale wanakunywa maji safi na salama, yale maji ya machafu
waliyokuwa wanakunywa siku zote muda si mrefu watasahau.
Ngoja
nirudi katika michezo Rais Samia umeweka nguvu kubwa katika Michezo yote
na tumeanza kuona matunda yake , umetuwekea goli la Mama ambalo hakika
timu zinavuna hela, huna baya mama, ni jambo la kawaida kuona kuona kapu
la fedha uwanjani.Wachezaji wanaogelea fedha tu na juzi umekuja na
Knock Out ya Mama,bondia Karim Mandonga amechukua fedha baada ya kumpiga
mpinzani wake Said Mbelwa.
Katika Utalii Rais Samia tunaona
matunda ya filamu yako ya Royal Tour, Utalii umeendelea kupaa nchini,
fedha za kigeni zinazotokana na utalii zimeendelea kuingia nchini.
Kuimarisha sekta ya utalii tunashuhudia hata Hadzabe nao wamekuwa
kivutio kikubwa baada ya kutangazwa.
Tunafahamu walikuwepo lakini
hakuna aliyekuwa akiwafuatilia lakini kupitia wewe leo wamekuwa maarufu
na wao wamekuwa kivutio kwa Watalii wanaokuja nchini na wanapiga Pesa.
Hata hivyo baada ya kueleza hayo naomba nikwambie na najua unajua Rais wangu unafahamu
kwa
mujibu wa Katiba yetu ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kila baada ya
miaka mitano tunafanya uchaguzi Mkuu kuchagua madiwani,Wabunge na
Rais,hivyo mwaka huu wa 2025 Watanzania tutakuwa na uchaguzi Mkuu.
Hivyo
ni mwaka wenye mishe mishe nyingi zinazohusu chaguzi,tutasikia
mengi,tutaona mengi lakini tumejiandaa nayo.Tunamuomba Mungu atuvushe
salama,tufanye uchaguzi uliojaa utulivu na amani.Ni matumaini yangu
Mungu yuko pamoja nasi wakati wote.
Kwa kuwa huu ni mwaka wa
uchaguzi najua kwa nafasi ya Rais Chama Cha Mapinduzi (CCM)
kitakusimamisha wewe Dk.Samia kugombea nafasi hiyo .Sina mashaka na wala
Watanzania hatuna shaka yoyote na uwezo wako kwani uliyoyafanya katika
uongozi wako umethibitisha uwezo wako, nchi iko salama na maendeleo
yamepatikana chini ya uongozi wako.
Kwa uwezo wako Dk.Rais Samia
ambaye pia ndio Mwenyekiti wa CCM Taifa sitarajii kuona akitokea
mwanaCCM mwingine akichukua fomu kwa ajili ya kugombea nafasi ya urais.
Najua
kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania mwana ccm
anaweza kuchukua fomu ndani ya Chama lakini kwa utaratibu wa Chama hicho
ambao umekuwepo kwa muda mrefu huwa Rais anapokaa kwa awamu ya moja
basi huachiwa aendelee na awamu ya pili kukamilisha awamu mbili za Urais
,miaka mitano awamu ya kwanza,miaka mitano mingine awamu ya pili.
Kwa
mujibu wa Katiba Rais atakaa miaka 10 kama watanzania wataridhia
kupitia sanduka la kura.Ni kweli Rais Samia ulichukua nafasi ya kuwa
Rais baada ya kifo cha Dk.John Magufuli lakini kwa mujibu wa utaratibu
Rais Samia ndio anayepewa nafasi tena ndani ya Chama hicho ili aendelee
kuwaongoza Watanzania.
Hivyo kwa utaratibu huo huo ambao
umekuwepo kwa muda mrefu na kuwa sehemu ya utamaduni wa CCM katika
salamu zangu kwako Rais Samia nakuomba wakati ukifika chakua fomu ya
Urais ndani ya Chama chako na binafsi katika uchaguzi Mkuu
tutakapojaaliwa afya na uzima basi kura yangu nikuhakikishie
inakusubiria wewe.Nisipokupa wewe nampa nani?
Kwa kazi kubwa na
nzuri ambayo umeifanya tangu uingie madarakani Watanzania tumeridhika na
uongozi wako na nina uhakika tutakuchagua wewe Rais Samia katika
uchaguzi Mkuu mwaka huu.
Watanzania wanakusubiria kwa hamu na
wameonesha dalili za ushindi wako Rais Samia mapema kabisa, tunakumbuka
mwaka 2024 nchi yetu imefanya uchaguzi wa Serikali za Mitaa na wagombea
wa CCM wameshinda kwa asilimia 99 .Ushindi huo wa CCM unathibitisha hamu
waliyonayo Watanzania kuwa Rais Samia utashinda katika uchaguzi Mkuu
mwaka huu kwa kishindo.
Niwaombe Wana CCM kuweka nguvu zao
katika kukupambabnia Dk.Samia urejee katika kiti cha Urais, sina shaka
na uimara wa Chama chako,sina shaka na mipango na mikakati ya CCM
linapokuja suala la uchaguzi.Katibu Mkuu Dk.Emmanuel Nchimbi anajua nini
cha kufanya.
Hata hivyo najua kwa hulka ya binadamu huwa
tunakuwa na matamanio na ndoto zetu na katika siasa wapo wanaotamani
kuwania Urais lakini kama kuna wana CCM wanaotaka nafasi hiyo ni vema
wakatumia hekima na busara wakakuacha Rais Samia uendelee kututumikia.
Ningeambia
niishauri CCM basi ushauri wangu ungekuwa katika uchaguzi Mkuu mwaka
huu kwa ngazi ya Chama fomu ya Mgombea Urais iwe moja kwa ajili ya Dk
Samia tu.Kwanza kutoa mafomu mengi kwa nafasi ya Urais ni matumizi
mabaya ya rasilimali fedha.
Rais Dk.Samia unatosha na mitano tena
ni jambo ambalo halina mjadala,wengine ndani ya CCM wasubiri 2030 kama
wanahitaji.Ninaposema hivi wanaoutaka Urais wananiona kama vile
nimechanganyiwa,wananiona mimi ‘Chawa’,wananiona Mnoko sana.Wananiona
sina uwezo wa kufikiria.Watu bwawa!!!
Niwaambie naeleza haya
nikiwa na akili zangu timamu na sijashawishiwa na mtu yeyote, kwanza ni
salamu zangu tu kwa Rais wewe unaumia nini? Au ndio unautaka
Urais?Kwanza hizo sifa unazo za kupambana na Dk.Samia?Hovyoo.
Mwaka
2025 ni mwaka wa Rais Samia ,iwe jua ,iwe mvua tuko naye.Najua kwa
mujibu wa Katiba nchi yetu iko katika Mfumo wa vyama vingi na tangu
mwaka 1995 vimekuwa vikishiriki uchaguzi Mkuu.
Hivyo katika
uchaguzi Mkuu mwaka huu wa 2015 navyo vinajipanga kwa ajili ya
kusimamisha wagombea katika nafasi ya madiwani,Wabunge na Rais lakini
kwa mtazamo wangu kwa nafasi ya Diwani na Mbunge huko tutajua wakati
ukifika watakaorudi sawa na wasiorudi sawa vile vile lakini kwa nafasi
ya Rais tunaenda na Samia tu.
Sifanyi kampeni na sina uwezo huo
lakini uliyoyafanya Rais yanathibitisha uwezo wako katika kulitumikia
Taifa.Lakini hata tukisema tunamchagua Rais kutoka upinzani nani anasifa
za kupambana na wewe Dk.Samia Suluhu Hassan au huyo Jamaa yao?
Wakati
nahitimisha salamu zangu kwako Rais Samia uniruhusu niwakumbushe
Watanzania kuhusu wewe kuwa ulizaliwa Januari 27, 1960 katika Kijiji cha
Kizimkazi, Mkoa wa Kusini Unguja. Umeolewa na Bw. Hafidh Ameir na
umejaaliwa watoto wanne, watatu wa kiume na mmoja wa kike.
Kuhusu
elimu na mafunzo Dk.Samia Suluhu Hassan ulipata elimu ya msingi katika
shule mbalimbali, zikiwemo Shule ya Msingi Chwaka iliyoko Unguja kuanzia
1966 hadi 1968, Shule ya Msingi Ziwani mwaka 1970 na Shule ya Msingi
Mahonda mwaka 1972. Baada ya hapo, ulijiunga na Shule ya Sekondari ya
Ng’ambo kwa ajili ya masomo ya Kidato cha Kwanza hadi cha tatu, na Shule
ya Sekondari Lumumba kwa ajili ya Kidato cha Nne kati ya mwaka 1973
hadi 1976.
Mwaka 1983, ulipata Astashada katika Mafunzo ya
Takwimu kutoka Chuo cha Uchumi, Zanzibar. Baada ya kufanya kazi kwa
kipindi kifupi kwenye Wizara ya Mipango na Maendeleo, mwaka 1983 hadi
1986, alijiunga na Chuo cha Maendeleo ya Uongozi Mzumbe (IDM) kwa ajili
ya masomo ya juu katika Utawala wa Umma.
Aidha, ulipita katika
Taasisi ya Chuo cha Utawala wa Umma Lahore, Pakistan 1987, Taasisi ya
Eastern and Southern African Management Institute (ESAMI) 1991, na
Taasisi ya Uongozi ya Hyderabad India 1998 kwa ajili ya Astashahada ya
Utawala.
Baada ya hapo, ulijiunga na Chuo Kikuu cha Manchester
kilichopo Uingereza kwa ajili ya masomo ya Juu ya Uchumi. Vilevile,
ulipata Shahada ya Uzamili ya Maendeleo ya Jamii kupitia programu ya
pamoja kati ya Chuo Kikuu Huria cha Tanzania na Chuo Kikuu cha Southern
New Hampshire, Marekani.
Kuhusu uzoefu ndani ya Serikali ni
kwamba Dk. Samia Suluhu Hassan ni Rais wa sita wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania ambaye pia ni Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM).
Uliapishwa Machi 19, 2021 kufuatia kifo cha ghafla cha aliyekuwa Rais wa
Awamu ya Tano, Hayati Dkt. John Pombe Joseph Magufuli.
Ndugu
Samia Suluhu Hassan wewe mwanamke wa kwanza nchini kushika nafasi za
Makamu wa Rais na hatimaye Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Nyadhifa
nyingine ulizoshika ndani ya Serikali ni; Waziri katika Ofisi ya Makamu
wa Rais anayeshughulikia mambo ya Muungano 2010/2015; Waziri wa Utalii,
Biashara na Uwekezaji katika Serikali ya Mapinduzi Zanzibar 2005/2010
na Waziri wa Kazi, Vijana, Ajira, Maendeleo ya Wanawake, na Watoto,
Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar mwaka 2000/2005.
Mwaka 2014,
ulihudumu kama Makamu Mwenyekiti wa Bunge lililojadili Katiba ya Jamhuri
ya Muungano wa Tanzania, na kuandaa rasimu ya Katiba mpya ya Tanzania.
Mwaka 1987 hadi 1988, alikuwa Afisa Mipango Rasilimali Watu na Mwaka
1977 hadi 1983, Karani Masijala.
Kwa upande wa uzoefu ndani ya
CCM ,Dk. Samia Suluhu Hassan uliingia katika siasa kama mwanachama wa
CCM tarehe 10 Juni, 1987. Uliingia katika siasa za uchaguzi mwaka 2000
katika nafasi ya Mjumbe wa Baraza la Wawakilishi wa Zanzibar kama
Mwakilishi wa Viti Maalum vya Wanawake hadi mwaka 2010.
Kwenye
Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2010, uligombea na kuchaguliwa kuwa Mbunge wa
Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ukiwakilisha jimbo la
Makunduchi, Zanzibar.
Mwaka 2002, ulichaguliwa kuwa Mjumbe wa
Halmashauri Kuu ya Taifa ya Chama cha Mapinduzi, na vile vile, kuteuliwa
kuwa Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chama cha Mapinduzi; nyadhifa ambazo
ameendelea kuzifanyia kazi hadi leo. Ndugu Samia ni Mjumbe wa Mkutano
Mkuu wa CCM Taifa, Mkutano Mkuu wa CCM Mkoa wa Kusini Unguja; na alikuwa
Mjumbe wa Kamati za Siasa Mkoa na Wilaya ya Kusini Unguja.
Kwa
upande wa Jumuiya za Chama cha Mapinduzi, Ndugu Samia wewe ni mwanachama
wa Jumuiya ya Wanawake wa Tanzania (UWT) kuanzia mwaka 1996 hadi leo.
Aidha, umeshiriki katika kuandika Ilani ya Chama cha Mapinduzi mara nne
mfululizo kuanzia 2005/2010, 2010/2015, 2015/2020 na 2020/2025.
Baada
ya maelezo hayo nitumie nafasi hii kukushukuru Rais Dk.Samia kwa kusoma
salamu zangu kwako,najua unaweza usisome kila kitu au kuweka yote
kichwani lakini bakia na hili tu Watanzania tunakupenda , tunakuombea
maisha marefu.Tunafurahia uongozi wako.Heri ya mwaka mpya wa 2025 Rais
Dk.Samia Suluhu Hassan ,Mama wa Taifa la Tanzania, tabasamu lako ndio
tabasamu letu Watanzania.
Ni mimi;0713833822