Meneja wa NSSF Mkoa wa Kinondoni,
Bw. Large Materu ametoa wito kwa wajasiriamali kuendelea kujiunga na
kujiwekea akiba katika Mfuko ili waweze kunufaika na mafao yanayotolewa
yakiwemo ya uzee, uzazi na matibabu.
Alitoa wito huo wakati
akiongoza utoaji wa elimu ya hifadhi ya jamii kwa viongozi wa masoko na
baadaye wafanyakazi wa NSSF waliweka kambi kwenye masoko ya Kawe na
Tegeta Nyuki kwa ajili ya kutoa elimu ya hifadhi ya jamii, kuandikisha
wanachama wapya, kuhamasisha uchangiaji ambapo hamasa ya wajasiriamali
kupata elimu na kujiunga imekuwa kubwa.
“Napenda kutoa wito kwa
wajasiriamali wote wakiwemo mama lishe, bodaboda, wakulima, wafugaji,
wavuvi kuwa NSSF ndio Mfuko wao, hivyo waendelee kujiunga na kujiwekea
akiba ili waweze kunufaika na mafao yote kama vile ya uzee, urithi,
uzazi na matibabu,” alisema.
Bw. Materu alisema NSSF imeweka
utaratibu mzuri wa wajasiriamali kujiunga na kuchangia ambapo mwanachama
baada ya kujiandikisha anapewa namba ya kumbukumbu ya malipo na
anapaswa kuchangia kuanzia shilingi 30,000 au 52,200 au zaidi kwa mwezi
na anaweza kuchangia kidogo kidogo kwa siku, wiki au mwezi ili aweze
kunufaika na mafao hayo.
Aidha, alisema NSSF imepiga hatua kubwa
katika utoaji wa huduma kwa wanachama na wananchi kwa kutumia mifumo ya
TEHAMA ambayo inarahisisha huduma. “Tunaishukuru Menejimenti ya NSSF kwa
kuweka nguvu kubwa sana katika kubadilisha mwelekeo wa utendaji kazi
kuwa wa kidijitali zaidi ambapo imepelekea wanachama na wananchi kwa
ujumla kupata huduma hukohuko waliko bila ya kulazimika kufika katika
ofisi za NSSF,” alisema Bw. Materu.
Alisema hayo ni mafanikio
makubwa na kuwa lengo la NSSF ni kuendelea kufanya maboresho zaidi ya
mifumo ili kumuwezesha mwanachama aweze kufungua madai ya mafao yake kwa
njia ya mtandao bila ya kulazimika kufika kwenye ofisi za Mfuko.