Na Mwandishi Wetu,
Dar
es Salaam. Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii
(NSSF), Bw. Masha Mshomba, tarehe 27 Januari 2025 amekutana na Waziri
Mkuu wa Jamhuri ya Uganda, Mhe. Robinah Nabbanja Jijini Dar es Salaam.
Akizungumza
mara baada ya kikao, Bw. Mshomba amesema Mhe. Robinah Nabbanja amefika
nchini kwa lengo kuhudhuria Mkutano wa Nishati wa Wakuu wa Nchi za
Afrika ambapo mbali na mkutano huo aliona ni vizuri kukutana na NSSF kwa
lengo la kufahamu mambo kadhaa kuhusu utendaji wa Mfuko ikiwa pamoja na
suala la ukuaji wa thamani ya Mfuko, uwekezaji, usajili wa wanachama wa
sekta binafsi na sekta isiyo rasmi na ulipaji wa mafao ya wanachama ili
kupata uzoefu.
“Kama
tunavyofahamu nchi yetu ya Tanzania imepata heshima kubwa kuwa mwenyeji
wa mkutano mkubwa wa Nishati wa Wakuu wa Nchi za Afrika na Mhe. Waziri
Mkuu wa Jamhuri ya Uganda amefika hapa nchini kwa lengo la kuhudhuria
mkutano huo, lakini ameona ni vizuri kuja kukutana na NSSF kwa lengo la
kufahamu masuala kadhaa ya utendaji ikiwemo uwekezaji unaofanywa na
NSSF, ulipaji wa mafao na masuala mengine ya huduma ikiwemo ushirikiano
kati ya NSSF Tanzania na ile ya Uganda’ na kwa kweli tumezungumzia hayo
ambayo aliomba tuyazungumzie na tumemueleza kwa mfano uwekezaji wetu
katika dhamana za Serikali, uwekezaji kwenye miundombinu mfano wa Daraja
la Nyerere Kigamboni, Kiwanda cha Sukari cha Mkulazi kule Morogoro na
miradi mengine ambayo NSSF imewekeza ikiwa ni pamoja na ile ya majengo”
alisema Bw. Mshomba.
Bw.
Mshomba pia alimueleza Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Uganda kuwa NSSF ipo
chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu, hususani kitengo cha Hifadhi ya Jamii
pamoja na Benki Kuu ya Tanzania na Ofisi ya Msajili wa Hazina kwenye
masuala ya uwekezaji.
Vile
vile, Bw. Mshomba alisema Mfuko umeimarika sana katika kipindi cha
miaka minne ya Serikali ya awamu ya sita chini ya Dkt. Samia Suluhu
Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ilipoingia madarakani.
“Katika
kipindi cha miaka minne ya uongozi wa Serikali ya awamu ya sita chini
ya Mhe. Rais wetu mpendwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, NSSF imepata
mafanikio makubwa ya utendaji hii inatokana na juhudi kubwa sana ya
serikali yake katika kuvutia wawekezaji nchini,” alisema Bw. Mshomba.
Alisema
kwa sababu NSSF inawafikia waajiri na wajiriwa katika sekta binafsi na
pia sekta isiyo rasmi, hivyo wawekezaji wanavyokuja nchini, inapelekea
ongezeko la wanachama, inaongeza waajiri, na hivyo kuongeza michango.
Aidha, uwekezaji na mapato yanayotokana na uwekezaji yamekuwa
yakiongezeka.
Bw.
Mshomba alimueleza Mhe. Robinah Nabbanja kuwa NSSF imeruhusiwa kuwekeza
nje ya nchi katika eneo la Afrika Mashariki, pia katika eneo la SADC,
ambapo kwa uwekezaji huo utasaidia kuongeza mapato ya NSSF kupitia
uwekezaji huo.
“Katika
uwekezaji huo tulioruhusiwa kuwekeza nje ya nchi, NSSF tumekuwa
tukishirikina na Mifuko mingine ya Hifadhi ya Jamii, mfano wenzetu wa
NSSF Uganda tunapofikiria kuwekeza katika HISA nchini Uganda ni lazima
tushirikiane nao kupata uzoefu wao katika soko la HISA la Uganda,”
alisema Bw. Mshomba.
Kwa
upande wa ushirikiano katika ya Mifuko miwili ya NSSF Tanzania na NSSF
Uganda ni mzuri kwani NSSF Tanzania imekuwa ikiwapa ushirikiano mzuri
NSSF Uganda hasa wanapokuja kuwekeza Tanzania, ambapo wao wameanza
kuwekeza katika dhamana za Serikali kwa muda mrefu.
“
Mheshimiwa Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Uganda amefurahi sana kuona
ushirikiano uliopo na wenzetu wa NSSF Uganda na akatoa rai kuwa ni
vizuri tukaendeleza ushirikiano huo kwa sababu si tu unajenga hizi
taasisi mbili bali unajenga nchi na unaimarisha uhusiano katika nchi na
nchi kitu ambacho ni muhimu hasa tunapofikiria kuendeleza Jumuiya ya
Afrika Mashariki na hilo amesisitiza sana na akaahidi atakaporudi nchini
Uganda ataweka msisitizo katika hilo.” aliongeza Bw. Mshomba
Kwa
upande wake, Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Uganda, Mhe. Robinah Nabbanja
aliipongeza NSSF kwa kazi nzuri wanayoifanya katika kuwahudumia
wanachama na Taifa kwa ujumla na kuomba ushirikiano uendelee kwa maslahi
mapana ya nchi zote mbili.