Mwaka 2025 umeanza kwa kishindo katika sekta ya utalii nchini Tanzania. Kwa mara ya kwanza katika historia, nchi imefanikiwa kuvuka lengo lake la kufikisha idadi ya watalii milioni 5 mapema zaidi kuliko ilivyotarajiwa. Kwa jumla, watalii 5,360,247 wameitembelea Tanzania, ikiwa ni ongezeko kubwa lililochangiwa zaidi na watalii wa ndani ambao wamefikia 3,218,352, huku watalii wa kimataifa wakiwa 2,141,895.
Katika hafla iliyofanyika jijini Dar es Salaam, tarehe 31 Januari 2025, Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Balozi Dkt. Pindi Chana, alitangaza mafanikio hayo makubwa kwa furaha na shukrani.
“Hili ni jambo la kihistoria. Ninatoa shukrani za dhati kwa Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kwa maono yake makubwa na uongozi wake thabiti. Kupitia jitihada zake, Tanzania imepata nafasi kubwa zaidi kwenye ramani ya utalii duniani, na tunazidi kuona matunda ya kazi hiyo kila siku,” alisema Waziri Chana.
Katika kipindi cha miaka michache tu, sekta ya utalii imepiga hatua kubwa. Watalii wa ndani wameonyesha mwitikio mkubwa zaidi kuliko ilivyowahi kushuhudiwa hapo awali. Kuongezeka kwa idadi hii kumetokana na kampeni mbalimbali za kuhamasisha utalii wa ndani, ikiwemo #UtaliiTena, pamoja na uwekezaji katika miundombinu ya vivutio vya utalii.
Pamoja na mafanikio haya, bado kuna kazi kubwa ya kufanikisha lengo la kuongeza mapato yatokanayo na utalii. Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii, Mhe. Timotheo Mnzava, ameipongeza Serikali kwa juhudi zake lakini akasisitiza kuwa bado kuna mwanya wa kuimarisha makusanyo.
“Tumevuka lengo la idadi ya watalii, lakini bado tunahitaji kusukuma mbele jitihada za kuongeza mapato. Kwa sasa tuko kwenye dola bilioni 4, lakini lengo letu ni kufikia dola bilioni 6. Tunahitaji mipango zaidi kuhakikisha tunafanikisha hili,” alisema Mhe. Mnzava.
Katibu Mkuu wa Maliasili na Utalii, Dkt. Hassan Abbasi, alibainisha kuwa Wizara imejipanga kimkakati kuhakikisha kuwa makusanyo ya dola bilioni 6 yanazidi kufikiwa ifikapo Desemba mwaka huu.
Serikali kupitia Wizara ya Maliasili na Utalii imejipanga kuimarisha huduma, kuboresha miundombinu, na kupanua masoko ya utalii ili Tanzania izidi kuwa kivutio kinachopendwa zaidi duniani.
Katika hafla hiyo, Waziri Chana aliwatambua na kuwapongeza wadau wote wa sekta ya utalii waliowezesha mafanikio haya.
“Kwa niaba ya Serikali, nawapongeza na kuwashukuru wote mliochangia mafanikio haya. Kazi yenu ni ya thamani kubwa, na tutaendelea kufanya kazi pamoja ili kuhakikisha mafanikio haya yanazidi kuimarika mwaka hadi mwaka,” alisema Waziri Chana.
Hafla hiyo ilihudhuriwa na viongozi mbalimbali kutoka Wizara ya Maliasili na Utalii, taasisi za serikali, mashirika binafsi, na wadau wa utalii.
Kwa mafanikio haya, Tanzania inaendelea kuthibitisha kuwa ni moja ya nchi zinazoongoza barani Afrika kwa vivutio vya utalii na huduma bora kwa wageni. Juhudi hizi zinaweka msingi imara wa maendeleo endelevu ya sekta hiyo kwa manufaa ya kizazi cha sasa na kijacho.