Na Silivia Amandius, Kagera
Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Bukoba na Diwani wa Kata ya Rukoma, Murshid Ngeze, amewataka viongozi wa ngazi zote—kuanzia kata, vijiji hadi vitongoji—kufanya kazi kwa mshikamano na ushirikiano ili kuharakisha maendeleo katika jamii.
Akizungumza wakati wa ziara yake ya siku moja Januari 31, 2024, katika Kata za Kibirizi na Rukoma, Mhe. Ngeze alisisitiza umuhimu wa umoja miongoni mwa viongozi, akibainisha kuwa ushirikiano wao ni nguzo muhimu kwa maendeleo, hasa kuelekea Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 2025.
Katika ziara hiyo, alikagua ujenzi wa Zahanati ya Kibirizi na kusikiliza changamoto zinazowakabili wananchi wa eneo hilo. Wananchi walieleza kuwa uhaba wa huduma za afya umekuwa kikwazo kikubwa, kwani wengi hulazimika kusafiri umbali mrefu kutafuta matibabu. Hali hii huzidi kuwa mbaya zaidi wakati wa mvua, ambapo baadhi ya wajawazito wamelazimika kujifungua njiani kutokana na ukosefu wa huduma za afya za karibu.
Mhe. Ngeze aliwapongeza wananchi na Mbunge wa eneo hilo kwa mchango wao katika ujenzi wa zahanati hiyo, akisema kuwa kukamilika kwake kutaleta suluhisho la kudumu kwa changamoto ya huduma za afya.
Aidha, alisisitiza kuwa mshikamano na ushirikiano baina ya viongozi na wananchi ni chachu ya mafanikio ya miradi ya maendeleo. Aliwataka viongozi kushirikiana kwa karibu ili kuhakikisha miradi inatekelezwa kwa wakati na kwa manufaa ya jamii.