Na. Benny Mwaipaja
Katibu Mkuu Wizara ya Fedha, Dkt. Natu El-maamry Mwamba, amekutana na kufanya mazungumzo na Mkuu wa Ushirikiano ambaye pia ni Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Usimamizi wa Uchumi Mpana na Fedha Mashariki na Kusini mwa Afrika (Macroeconomic and Financial Management Institute of Eastern and Southern Africa- MEFMI), Dkt. Louis Kasekende, ambapo pamoja na mambo mengine, wamejadiliana namna Taasisi hiyo inavyoweza kuandaa mafunzo maalumu katika nyanja za kiuchumi, Akili Mnemba (Artificial Intelligence), na uchumi wa kijani ili kuiwezesha nchi kuwa na wataalam waliobobea katika nyanja hizo ili kuisaidia nchi kupata suluhisho la mabadiliko ya kiuchumi yanayotokea duniani kutokana na kasi ya ukuaji wa teknolojia na mabadiliko ya sera za misaada na mikopo kutoka nchi zinazoendelea.
Kikao hicho kilichofanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa Katibu Mkuu-Hazina, Jijini Dodoma, kimemshirikisha pia Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania, Bw. Emmanuel Tutuba, Baadhi ya Menejeimenti ya Wizara ya Fedha, Benki Kuu ya Tanzania, pamoja na MEFMI.
Macroeconomic and Financial Management Institute of Eastern and Southern Africa (MEFMI), ni Taasisi ya Kikanda inayojihusisha na utoaji mafunzo kwa nchi wanachama wake katika kuwajengea uwezo wa uendeshaji wa program za maendeleo, katika usimamizi wa Uchumi Mpana na Usimamizi wa Fedha.






