Mkurugenzi wa shirika la Immacate Foundation Emmanuel Ntobi akizungumza kwenye hafla ya uzinduzi wa vyoo iliyofanyika katika Kata ya Shibula Wilaya ya Ilemela Jijini Mwanza

Wakanza kulia ni Rahel Mwanale miongoni mwa wanufaika waliojengewa vyoo na Shirika la Immacate Foundation akiwa amekaa na Mkurugenzi wa shirika hilo Emmanuel Ntobi kushoto pamoja na Mtendaji wa Kata ya Shibula Petro Mwaisamila.

Choo cha awali walichokuwa wanatumia familia ya Rahel Mwanale ambae ni mzee mwenye ulemavu

Choo kilichojengwa kwenye familia ya Rahel Mwanale ambae ni mzee mwenye ulemavu ambacho ni miongoni mwa vyoo 10 vilivyojengwa na shirika la Immacate Foundation katika Wilaya ya Ilemela na Nyamagana Jijini Mwanza.
………….
Na Hellen Mtereko, Mwanza
Baadhi ya familia zenye wazee wenye ulemavu Mkoani Mwanza zimejengewa vyoo ambavyo vinakidhi mahitaji maalum kwa wazee hao hatua itakayosaidia kuepukana na magonjwa ya mlipuko ikiwemo kipindupindu.
Immacate Foundation imejenga jumla ya vyoo 10 ambapo katika Wilaya ya Ilemela ni vyoo sita na Nyamagana vinne.
Immacate Foundation ni shirika lisilo la kiserikali lenye makao yake makuu Jijini Mwanza na limejikita katika kuwahudumia watoto wenye ulemavu Tanzania kwakuwapa elimu na vifaa saidizi.
Akizungumza katika hafla ya uzinduzi wa vyoo hivyo iliyofanyika Feburuari 6, 2024 katika Kata ya Shibula Wilaya ya Ilemela Mkoani Mwanza Mkurugenzi wa Immacate Foundation, Emmanuel Ntobi, alisema wamejenga vyoo hivyo kwa lengo la kuboresha hali ya maisha ya watu wenye ulemavu na kuhakikisha wanapata huduma bora za kijamii.
Amesema Immacate Foundation imekuwa mstari wa mbele katika kutekeleza miradi inayolenga kusaidia jamii,hususani makundi maalum kama watu wenye ulemavu.
“Vyoo hivi vitatoa fursa kwa wazee wenye ulemavu kutumia miundombinu salama yenye hadhi na inayowajali na hivyo kuboresha afya zao na kuongeza heshima yao katika jamii”, amesema Ntobi
Aidha, alisema kuwa wanatambua mchango mkubwa wa Serikali katika kuboresha maisha ya watu wenye ulemavu na kuhakikisha usawa katika upatikanaji wa huduma muhimu.
Alisema pamoja na mafanikio hayo yote bado wanakabiliwa na changamoto kadhaa ikiwemo kupanda kwa bei za vifaa vya ujenzi vinavyopelekea kuathiri bajeti ya miradi yao.
“Bado kunauhitaji mkubwa wa vyoo zaidi ili kukidhi mahitaji ya watu wote wenye ulemavu katika maeneo mengine,vilevile ufadhili katika huduma za kijamii umekuwa mdogo jambo linalozuia upanuzi wa miradi muhimu kama hii, hivyo tunaamini kupitia ushirikiano na wadau mbalimbali pamoja na Serikali changamoto hizi zinaweza kupatiwa suluhisho la kudumu”,
Tedy Nicolaus ni mtoto wa Rahel Mwanale ambae ni mzee mwenye ulemavu wa miguu na mnufaika wa mradi wa vyoo hivyo amesema awali mama yake alikuwa anajisaidia kwenye ndoo akisha maliza wanaenda kumwaga kwenye shimo la choo cha zamani ambapo ilikuwa ni ngumu mama huyo kwenda kujistiri.
“Nilikuwa nambeba mama namkalisha kwenye ndoo kwaajili ya kujisaidia akimaliza naenda kumwaga kwenye choo cha zamani ambacho kilikuwa siyo choo bora hata kwetu sisi ambao ni wazima”, alisema Nicolaus
Ameishukuru Immacate kwakuwajengea choo kizuri na cha kisasa ambacho kitawaletea heshima kubwa kwenye familia yao.
Kwa upande wake Maria Mussa ambae ni jirani wa familia hiyo alisema awali familia hiyo ilikuwa inapata shida sana kwenye kujistri kutokana na kutokuwa na choo kinachokidhi mahitaji lakini kwa sasa baada ya kujengewa choo na taasisi ya Immacate watajistiri katika mazingira mazuri.
Akizungumza mara baada ya uzinduzi wa vyoo hivyo Mtendaji wa Kata ya Shibula Wilaya ya Ilemela Mkoani Mwanza, Petro Mwaisamila alisema Kata hiyo inajumla ya watu wenye ulemavu 36 kwamujibu wa sensa ya watu na makazi ya mwaka 2022 huku idadi hiyo ikitajwa kuongezeka kutokana na idadi ya watu wanavyoendelea kujenga.
Alisema shirika la Immacate limefanya jambo zuri la kuwakumbuka wazee wenye ulemavu kuwajengea miundo mbinu mizuri ya vyoo huku akiongeza kuwa hatua hiyo inaunga mkono juhudi za Serikali.