NA VICTOR MASANGU, KIBAHA
MKE wa Mbunge wa Jimbo la Kibaha mjini, Selina Koka ameimiza jumuiya ya wanawake kuhakikisha kwamba wanakuwa na umoja na mshikamano ili kuwa na misingi imara na kumpa sapoti ya kutosha Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan aweze kushinda kwa kishindo kwenye uchaguzi mkuu mwaka 2025.
Koka ameyasema hayo katika Kikao cha Baraza la Jumuiya ya Wanawake Kibaha vijijini kilichofanyika na kuhudhuliwa na viongozi mbali mbali wa chama na jumuiya zake kwa lengo la kujadili mambo mbali mbali ikiwemo suala zima la kujiandaa na uchaguzi mkuu wa mwaka 2025.
Katika hatua nyingine amewahimiza wanawake wa jumuiya hiyo kuanzia ngazi za matawi kuhakikisha wanajitokeza kwa wingi katika zoezi la uboreshaji wa daftari la kudumu la wapiga kura ambalo linatarajiwa kuanza kufanyika rasmi Februari 13 hadi 19 mwaka huu lengo ikiwa ni kupata fursa ya kupiga kura.
Aidha, Mama Koka amempongeza Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuweza kutenga fedha nyingi ambazo zimeweza kwenda kufanya mambo makubwa katika kutekeleza miradi mbali mbali ikiwemo afya, elimu, maji, pamoja na huduma za kijamii.
Kwa upande wake mjumbe wa Halmashauri ya chama cha mapinduzi CCM Taifa kupitia Jumuiya ya Wazazi (MNEC) Hamoud Juma amewataka wanawake kuunda kamati za ushindi kuanzia ngazi za matawi kwa lengo la kuweza kumpa kura nyingi Rais Samia katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2025.